Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt. Peter M. Nyanja kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya Serikali.
Mhe. Majaliwa ametoa pongezi hizo katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tabora ambapo ambapo alitembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwamo jingo la Utawala la Manispaa ya Tabora
Aidha Mhe. Majaliwa katika kikao na Viongozi pamoja na Watendaji wa Mkoa wa Tabora amepokea Salamu za Mkoa wa Tabora kutoka kwa Mkuu wa Mkoa Dkt. Batilda Burian ambapo pamoja na mambo mengine amemshukuru sana Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa upendeleo wake mkubwa kwa Mkoa wa Tabora.
Kwani zaidi ya Bilioni mia moja na kumi (110) zimetumika kwenye miradi ya maendeleo Mkoani Tabora kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na kwa upande wa Manispaa ya Tabora ikipata zaidi ya Bilioni nane (8) kwenye miradi yake maendeleo.
Katika Manispaa ya Tabora Mhe. Majaliwa amepata fursa ya kuongea na Wananchi na Watendaji wa Serikali na kueleza namna gani Serikali ya awamu ya sita imejipanga kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Na baadae amekagua mradi wa Jengo Jipya la Utawala linalojengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu, Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi imara wa Mama Samia Suluhu Hassan jingo ambalo kwa sasa liko hatua ya umaliziaji.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Tabora kuwekeza kwenye miradi yenye tija, ya kimkakati na yenye kuleta matokeo chanya kwa mapato yao ya ndani,kwani miradi mingi inayotekelezwa ni midogomidogo na haina tija sana kwa Halmashauri husika.
Mhe.Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuongeza tija, ubunifu na mbinu za kukusanya mapato ya ndani ili waweze kutoa huduma bora kwa Wananchi. Vilevile amewataka kufuata sheria na taratibu za matumizi ya fedha hizo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha zinapelekwa kwanza benki ndio zirudi kufanya matumizi.
Aidha katika kipengele cha mapato amesisitiza mawakala wapewe mikataba na ikiwa ni baada ya kufanya tathimini ya kina kwenye vyanzo husika, hii ikiwa ni kuleta ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Aidha katika hotuba yake Mhe.Kassim Majaliwa amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha fedha zote ambazo hazijaingia kwenye akaunti husika benki katika Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora zinapelekwa haraka iwezekanavyo na vinginevyo achukue hatua muhimu ikiwa ni pamoja na kushirikisha vyombo vingine vya Serikali ikiwamo TAKUKURU.
Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. John Mbowe kufanya msawazo wa watumishi ndani ya Mkoa wa Tabora ikiwa ni kupambana na uhaba wa Watumishi kwani kuna Halmashauri zingine zinakuwa na watumishi wengi katika kada flani huku Halmashauri nyingine zikiwa na uhaba mkubwa wa watumishi wa kada kam hiyo hiyo.
Waziri Mkuu amewaagiza Meya na Wenyeviti wa Halmashauri wawe wakali kwenye matumizi ya fedha za Halmashauri na wahakikishe taratibu na kanuni zinafuatwa ambapo ameeleza kwamba Baraza la Madiwani linawajibu wa kuhakikisha kwamba kila shilingi inatumika kulingana na bajeti iliyopangwa na sio vinginevyo, na kuhakikisha kwamba sheria na taratibu zote zinafuatwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt Peter Maiga Nyanja wakati akielezea utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jingo la utawala amesema kwamba mpaka sasa jengo linahitaji zaidi ya Bilioni mbili ili kuweza kukamilika kabisa, ambapo Mhe. Majaliwa ameahidi Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaipatia Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Bilioni moja kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ili kuendelea kukamilisha jengo hilo kwa sababu Mkurugenzi na Manispaa ameweza kusimamia vyema matumizi ya fedha za awali.
Mwisho kabisa Mhe.Kassim Majaliwa amewashukuru Wananchi wa Tabora kwa mwitikio wao mkubwa kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lakini vilevile kwa ukarimu wao na mapokezi makubwa wakati alipokuja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kwamba upendo wa watu wa Tabora unawapa nguvu wao kama Viongozi wa Serikali.
MWISHO.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.