Na Alex Siriyako:
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu wa 2025, Ndugu Ismail Ali Ussi, ameeleza kukoshwa na ubora wa miradi ya maendeleo iiliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Ndugu Ussi ametoa maelezo haya leo Julai 30, 2025 ambapo amepata fursa ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa ya Tabora.
Ikumbukwe kuwa, Wilaya ya Tabora imeupokea Mwenge wa Uhuru na kuukimbiza leo Julai 30,2025 ambapo Mwenge wa Uhuru umeangazia miradi minane yenye thamani ya zaidi ya bilioni kumi na tisa (19) katika kata za Itetemia, Kitete, Ipuli, Mtendeni, Isevya, Misha pamoja na Cheyo.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru ni Kituo cha Afya Itetemia, Kikundi cha Vijana cha asilimia kumi cha KAZI DIGITAL, Barabara ya Maili Tano, Kiwanda cha Kuchakata Nishati Mbadala cha Gereza Kuu la Uyui, Ofisi ya Kata ya Isevya, Chanzo cha Maji cha Bwawa la Igombe, pamoja na madarasa ya Wanafunzi wenye mahitaji maalumu shule ya Sekondari Kazima.
Ndugu Ismail Ali Ussi kwa nyakati tofauti tofauti akiongea na Wananchi kwenye miradi na maeneo ya ujumbe wa Mwenge wa uhuru, amewaomba na kuwahimiza kuendelea kuwa wazalendo, waendelee kuchapa kazi, waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya maradhi kama Malaria, Ukimwi, kubwa zaidi akasisitiza Wananchi kujitokeza kuwachagua viongozi wanaowapenda ifikapo Oktoba mwaka huu kwa utulivu na amani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe.Upendo Wela amemshukuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi kwa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyopo katika Manispaa ya Tabora.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2025
"JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU."
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.