Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela ameeleza kuwa, kila mfanyabiashara awe mkubwa, wa kati na mdogo katika Manispaa ya Tabora anao wajibu wa kulipa ushuru, kodi na tozo mbalimbali zilizopo kwa mujibu wa sheria mama ya Nchi na sheria ndogo ya Halmashauri.
Mhe. Kapela ametoa rai hii leo mei 20, 2025 wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024/2025, kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora.
Mhe. Kapela ametoa maelezo haya kufuatia baadhi ya wafanyabiashara waliopisha ujenzi wa soko kuu na kuhamishiwa eneo la nyuma ya stendi mpya kugoma kulipa kodi ya pango ya Tsh.50,000/= kwa kibanda na kudai kuwa wao wapo tayari kulipa Tsh.20,000/= kwa kibanda. Mhe. Kapela amefafanua kuwa, kodi ya pango hupangwa kulingana na bei ya soko na kiasi cha elfu hamsini wanachotakiwa kulipa ni kidogo sana ukilinganisha na bei ya soko ya eneo hilo.
Aidha, Mhe. Kapela ameeleza kuwa, Manispaa ya Tabora imepata mwekezaji ambae ameonesha nia ya kuwekeza kiwanda cha mbolea na yuko katika mazungumzo na Serikali na ameongeza kuwa, kuna mwekezaji mwingine anaetaka kuwekeza kwenye kiwanda cha kusindika viazi vitamu, hivyo Manispaa ya Tabora itapiga hatua kubwa sana kwa uwekezaji huu.
Kadhalika katika Baraza hili, wajumbe na waalikwa wamepata fursa ya kupata elimu ya BIMA YA AFYA KWA WOTE kutoka kwa Meneja wa NHIF Mkoa wa Tabora Ndugu Salum Adamu.
Ndugu Adam ameeleza kuwa, Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata haki ya kupata matibabu, imekuja na mpango thabiti wa utekelezaji wa ajenda hiyo, ambao ni BIMA YA AFYA KWA WOTE.
Ameeleza kuwa bima hii inatolewa kwa kaya ambapo Baba, Mama na watoto wanne watapata bima hii kwa kiasi cha Tsh. 150,000.00 kwa mwaka mzima, na mtu mwenye bima hii ana nafasi ya kitibiwa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma vya umma na binafsi, tena kwa ngazi zote kwa maana ya ngazi ya kituo cha afya hadi Hospitali ya rufaa ya Taifa.
Ndugu Adam ameeleza kuwa, kwa sasa wakazi wa Mkoa wa Tabora bado wanachangamoto ya kukata bima pindi wanapata shida ya kuumwa, jambo linalokwenda kinyume na sera ya bima ambayo inataka Wananchi wote wakate bima, ili iwe rahisi kumhudumia mwenye uhitaji kwa urahisi na haraka.
Ndugu Elias Kayandabila, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora ameeleza kupokea maelekezo na ushauri wa wajumbe wa Baraza la Madiwani, lakini pia ameungana na Meneja wa NHIF Mkoa wa Tabora kuwataka Wakazi wa Manispaa ya Tabora kukata bima hii “BIMA YA AFYA KWA WOTE”, kwani maradhi yanamkuta mtu mwenye kipato hata cha chini, tena akiwa hajajipanga, hivyo bima hii ni mkombozi wa wanyonge
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.