Na Alex Siriyako:
Chifu Msagata Fundikira, Mtemi wa Unyanyembe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Machifu Tanzania ameongoza mamia ya wakazi wa Manispaa ya Tabora kumuombea Dua maalumu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Dua hii maalumu imesomwa leo Julai 12, katika viwanja vya Ikulu ya Unyanyembe na kuhudhuriwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali, viongozi wa Chama, Machifu wa Mkoa wa Tabora, Viongozi wa makundi maalumu, pamoja na Wakazi wa Manispaa ya Tabora.
Chifu Fundikira ameeleza kuwa, Tanzania ni Nchi yenye amani, na amani hii inadumishwa na Wananchi kwa kushirikiana na Viongozi wetu, hivyo kwa kutambua kuwa tunaelekea kwenye chaguzi za kuwapata viongozi wetu ifikapo Oktoba mwaka huu, Rais wetu kama kiongozi Mkuu wa Nchi anakabiliwa na jukumu kubwa, na hivyo kuna haja ya kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema, hekima na busara, ili aweze kutuvusha salama katika kipindi hiki.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt.John Mboya, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ndugu Paul Chacha, amemshukuru sana Chifu Fundikira kwa kuandaa Dua maalumu ya kumuombea Kiongozi wetu Mkuu wa Nchi, kwani mzigo alionao ni mkubwa sana, kama Watanzania tuna wajibu wa kumuombea kwa Mwenyezi Mungu.
Aidha, Dkt.Mboya amewaasa Watanzania kudumisha amani na upendo hasa kwenye nyakati hizi za uchaguzi, na ameongeza kuwa madhara yatokanayo na uvunjifu wa amani sio lazima yafundishwe shuleni, tunaweza kujifunza kwa Nchi jirani ambazo amani imetoweka.
Vilevile Dkt.Mboya amewaomba Wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ifikapo Oktoba mwaka huu, watumie haki zao za kikatiba kuwachagua viongozi wanaowapenda kwa ngazi za Rais, Wabunge na Madiwani.
Dkt.Mboya ametanabaisha vilevile kazi kubwa ya kuleta maendeleo kwa Wananchi ambayo imefanywa na Serikali ya awamu ya sita katika sekta za afya, elimu, kilimo,mifugo, pamoja na miundombinu ya barabara na maji.
Katika kuhitimisha ujumbe wake, Dkt.Mboya ameahidi kufikisha ombi la wakazi wa Tabora kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibari Mhe.Hussein Mwinyi, ombi la kuukarabati uwanja wa Ali-Hassan Mwinyi, ikiwa ni ishara ya kuendelea kumuenzi Hayati Ali-Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya pili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Dkt.John Pima, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kwa upande wake ameungana na viongozi wengine kuishukuru familia ya Chifu Fundikira kwa kuandaa Dua hii maalumu, na ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi na Wananchi wa Tabora wampe ushirikiano, ili kwa pamoja waweze kuendelea kuchagiza maendeleo ya Tabora na Tanzania kwa ujumla.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.