Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe.Upendo Wella amewatunuku vyeti vya pongezi walimu waliofanya vizuri katika masomo wanayofundisha kwenye mitihani ya Kitaifa ya Kidato cha sita ya mwaka huu wa 2025.
Walimu hao ni pamoja na Mwalimu Munira Ally Omari kutoka shule ya Tabora Wavulana ambae somo lake la General Studies (elimu ya Uraia) limechukuwa nafasi ya kwanza Kitaifa, Mwalimu Hamisi Omar Chingwalu kutoka Shule ya Tabora Wavulana ambae somo analofundisha la Kemia limechukua nafasi ya pili kitaifa, pamoja na Mwalimu John Lugonda Dotto kutoka Shule ya Tabora Wavulana ambae nae pia somo lake la Fizikia limechukua nafasi ya pili kitaifa.
Walimu wengine ambao wametunukiwa vyeti ni pamoja na Mwalimu Irene Lusungu Malekela kutoka Shule ya Tabora Wavulana ambae somo lake la Hesabu limepata nafasi ya pili kitaif , Mwalimu Rose Albert Mwaifunga kutoka shule ya Sekondari Kazima ambae somo lake la lugha ya Kiswahili limepata nafasi ya pili Kitaifa, na Mwalimu Getruda Alfred Ndogole kutoka shule ya sekondari Tabora Wavulana, somo lake analofundisha la Biolojia limeshika nafasi ya pili Kitaifa.
Aidha Mhe.Wella amezitunuku vyeti shule za sekondari za Tabora Wavulana pamoja na Shule ya Kazima kwa kufanya vizuri kwa ujumla katika mitihani ya kidato cha sita ya mwaka huu wa 2025, kwani shule ya Tabora Wavulana imekuwa ya pili Kitaifa, huku watahiniwa wote wakipata daraja la kwanza, na shule ya Kazima imeonesha mwenendo mzuri sana kwa watahiniwa wa shule hiyo 229 kupata daraja la kwaza ukilinganisha na mwaka 2024 ambapo watahiniwa 80 tu ndio walipata daraja la kwanza.
Mhe.Wella akiongea na Walimu wa Manispaa ya Tabora katika viwanja vya shule ya Tabora Wavulana ambapo walijumuika katika kongamano la MWALIMU DAY, kongamano ambalo limeratibiwa na benki ya NMB, ameeleza kuwa, mafanikio haya yaliyopatikana ni muunganiko wa mambo mengi ikiwa ni pamoja na jitihada za Serikali kuwekeza Miondombinu ya kutosha kwenye sekta ya Elimu, jitihada za Walimu pamoja na wanafunzi wenyewe.
Na Alex Siriyako:
Ameongeza kuwa, bado kama Wilaya ya Tabora tunayo shauku ya kufanya vizuri zaidi ya hapo, nguvu tunazo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kazi ikiwa ni sambamba na stahiki za watumishi, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuyamudu vyema majukumu yake.
Amewashukuru NMB kwa kuandaa kongamano ambalo limewakutanisha Walimu wote, kwani walimu wanapokutana wanapata mwanya wa kubadilishana uzoefu.
Aidha, Mhe.Wella amewapongeza walimu waliofanya vizuri na shule zilizofanya vizuri, na amewataka walimu na shule zingine zihamasike sasa na matokeo ya shule hizi za Tabora Wavulana na Kazima.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. John Pima ameeleza kuwa, wao kama Manispaa ya Tabora wanaendelea kujipanga vizuri zaidi, ili mitihani inayofuata shule nyingi ziweze kufanya vizuri zaidi.
Dkt. Pima ameongeza kuwa, Serikali ya awamu ya sita imeleta fedha nyingi sana za kujenga miundombinu katika shule zote za Manispaa ya Tobora, hivyo mazingira ya kujifunzia yameboreshwa sana, kinachotakiwa sasa ni muunganiko wa jitihada za Walimu, Wazazi na Wanafunzi wenyewe, kila mmoja aweke mikakati yake vizuri na kuitekeleza.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.