Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemeni Jafo (MB) ametembelea na kukagua ujenzi wa barabara za Lami zenye urefu wa KM 21.3
Katika ziara hiyo Mhe Waziri alikuwa ameongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya TARURA TANZANIA, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri, Mbunge wa Tabora Mjini Mhe Adamson Mwakasaka, Viongozi mbali mbali wa Manispaa ya Tabora ambapo walitembelea na kukagua ujenzi wa mtandao wa barabara kwa kiwango cha Lami na kuridhishwa kwa namna ambavyo ujenzi huo ulivyofanyika na viwango vyake.
''Nimekuwa ziarani kwa siku sita sasa, nimetembelea na kukagua miradi yote ambayo ipo chini ya Wizara yangu ya TAMISEMI kwa mikoa saba ikiwemo na Tabora kwenye Manispaa yenu ya Tabora ambapo nimekagua na kuridhishwa sana na mradi huu wa ujenzi wa barabara KM 21.3 kwa kiwango cha Lami, huu ni moja ya mradi uliotumia fedha nyingi sana chini ya Mradi wa Kimkakati wa Uimarishaji Halmashauri za Miji na Manispaa (ULGSP) hakika nimeridhishwa HONGERENI SANA MANISPAA YA TABORA,'' alisema Mhe Jafo.
Waziri Jafo alisema kuwa yote hayo ni matokeo na matunda ya kazi kubwa inayofanywa na Mhe John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Tanzania kwa wananchi wake, na kwamba hawakukosea kumchagua Mhe Rais, kwa msingi huo kuna kila sababu ya kumshukuru Mhe Rais wetu.
Aidha katika hatua nyingine Mhe Jafo aliwaambia wananchi wa Manispaa ya Tabora waliokuwa wakimsikiliza kwenye mkutano huo wa hadhara kwamba, kupitia Mbunge wa Tabora Mjini Mhe Mwakasaka na baadhi ya Waheshimiwa Madiwani walienda kumfuata Ofisini kwake Dodoma na kumuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo aliwaahidi kuwapatia kiasi cha Shilingi Bilioni Moja.
Kwa upande wa Elimu, Mhe Jafo aliwaeleza wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ilitoa kiasi cha Bilioni 89 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe Nchi nzima zikiwemo na shule za Tabora Wavulana, Milambo Wavulana na Kazima Sekondari zote hizi zipo hapa Tabora Manispaa.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa ULGSP, Meneja wa TARURA Tabora Manispaa Mhandisi Edwin Kabwoto alimueleza kuwa Mradi huo wa Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami nene umejengwa kwa awamu tatu tofauti (Three phases).
Ambapo awamu ya kwanza (LOT 1 sawa KM 6.1 ujenzi) ulifanyika chini ya ya Mkandarasi M/S SALUM MOTORS TRANSPORT Co LTD na ANAM ROAD WORKS Co Ltd, awamu yapili (LOT 2 sawa na KM 9.23) Mkandarasi alikuwa M/S SALUM MOTORS Co LTD na ANAM ROAD WORKS Co Ltd na awamu ya tatu (LOT 3 sawa na KM 6.02) Mkandarasi alikuwa ni CHONQING International Construction Corporation (CICO) na hivyo kukamilisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa KM 21.3
Kukamilika kwa mradi huu katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kumeongeza tija katika uzalishaji, usafirishaji wa bidhaa na abiria kutoka eneo moja kwenda lingine pia umesaidia kuboresha muonekano wa Mji na kuongezeka kwa thamani ya maeneo yaliyokaribu na barabara hizo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.