Waziri Ofisi ya Rais - Tamsemi Seleman Jafo, ameupongeza mkoa wa Tabora kwa kufanya vizuri kielimu katika kipindi kifupi kilichopita.
Akizungumza na wanafunzi wa shule ya msingi Ipuli, iliyopo Manispaa ya Tabora, alisema amefurahishwa na maendeleo na matokeo mazuri kitaaluma katika mkoa wa Tabora.
Alisema mkoa una sifa kubwa kielimu na katika mapambano ya kudai Uhuru huku zikiwepo shule kongwe za Tabora wavulana na wasichana ambazo zimekarabatiwa kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya kufanya vizuri kitaaluma.
Ukarabati wa shule haufanyiki tu kwa shule kongwe bali hata zile za kata ambazo zimefanya vizuri kitaaluma kwani mwaka huu zimeshika nafasi 52 katika nafasi 100 bora.
Akiielezea shule hiyo ya Ipuli, alisema wataangalia namna ya kuiwezesha ili ipate madarasa kwa vile kuna msongamano mkubwa wa wanafunzi.
“Tutaangalia chochote na fursa itakayopatikana kupata fedha za kuongeza nguvu katika madarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani kwenye shule hii ya Ipuli”Alisema Waziri Jafo.
Waziri Jafo alikuwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora kwenye wilaya za Igunga na Nzega kuhusiana na shule shikizi ambazo ni maalum kwa ajili ya wanafunzi wanaoishi mbali na shule mama.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.