Mke wa Rais Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa wametoa wito kwa Watanzania kujijengea utamaduni wa kutembelea vituo vya wazee na watu wenye mahitaji maalumu na kutoa misaada ili waweze kujikimu.
Wameyasema hayo leo (Jumatano, Februari 15, 2017) wakati walipotembelea Makazi ya Wazee wasiojiweza na walemavu watokanao na ugonjwa wa ukoma ya Amani Ipuli yaliyoko kwenye Manispaa ya Tabora mkoni Tabora. Katika makazi hayo wamekabidhi tani 7.5 za vyakula mbalimbali ukiwemo mchele, unga wa sembe na maharage pamoja na mafuta maalumu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa ngozi wanaosoma katika shule mbalimbali mkoni Tabora.
Hata hivyo, Mama Janeth amewapongeza watumishi wote wanaofanyakazi kwenye makazi ya kulelea wazee na watu wenye mahitaji maalumu kwa sababu kazi hiyo ni ngumu na ina changamoto nyingi. “Ibada si kwenda katika nyumba za ibada pekee bali hata kuwatembelea wazee, watu wenye mahitaji maalumu na wasiojiweza utakuwa umetoa sadaka kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Nawaomba tujitahidi kuwatembelea,” amesema.
Kwa upande wake Mama Mary amewaomba wananchi wote wawe na utaratibu wa kuwasaidia wazee wanaoishi katika makaazi ya kulele wazee, walemavu na wasiojiweza nchini na kuwafariji kwa sababu wanahitaji upendo na faraja kutoka kwao.
Pia Mama Mary ameipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau mbalimbali kwa kujitoa kwa hali mali katika kuwahudumia wazee na watu wenye mahitaji maalumu. Naye Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala amesema Serikali itahakikisha huduma zinaboreshwa katika makazi ya kulelea wazee na watu wenye mahitaji maalumu nchini kwa kuwa vingi viko katika hali mbaya.
Awali Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Tabora, Bw. Baraka Makona alisema makazi hayo yalianzishwa mwaka 1969 kwa lengo la kuwasaidia watu wasiojiweza hususan walioathirika na ugonjwa wa ukoma ambao walitengwa na familia zao.
Bw. Makona alisema baada ya ugonjwa wa ukoma kupungua mkoani Tabora kwa sasa makao hayo yanahudumia wazee wasiojiweza wenye ulemavu na ambao wametengwa na jamii kutokana na sababu mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Bw. Makona alisema makazi hayo yanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za uchakavu wa majengo, ukosefu wa gari la wagonjwa hali inayosababisha usumbufu mkubwa hasa inapotokea dharura nyakazi za usiku kwani hakuna zahanati karibu na makazi hayo.
Pia Bw. Makona amewapongeza wake wa viongozi hao kwa moyo wao wa dhati wa kuamua kutembelea makazi hayo na kutoa misaada mbalimbali vikiwemo vyakula kwa sababu wameonyesha matendo ya huruma na Mwenyezi Mungu atawabariki.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.