Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Komanya Kitwala leo tarehe 25/9/2019 amefanya ziara kwenye shule za Sekondari za NKUMBA iliyopo Kata ya Uyui na Sekondari ya CHANG’A iliyopo Kata ya Tumbi kwa ajili ya kukagua maeneo yatakayo jengwa madarasa ya kidato cha tano na sita ifakapo 2020.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo kwenye Shule ya Sekondari NKUMBA aliwaambia walimu, wajumbe wa bodi ya shule pamoja na wataalamu wa Elimu aliokuwa ameongozana nao kuwa, amekwenda kuangalia na kujiridhisha eneo litakalojengwa madarasa kwa ajili ya kidato cha tano na sita na mabweni mawili kwa ajili ya watoto wa kike.
‘’Ninao mpango mkubwa wa kufanya mapinduzi makubwa ya kielimu kwa Manispaa ya Tabora ikiwa ni sehemu ya ahadi yangu tangu nilipofika hapa Manispaa ya Tabora kwamba nitahakikisha naanzisha kidato cha tano na sita Shule mbili za NKUMBA na CHANG’A chini ya usimamizi wangu kama Mkuu wa Wilaya ili niweze kumsaidia Mhe Rais Dk John Pombe Magufuli kwenye adhima yake ya kuinua Elimu nchini kama alivyoahidi akiinadi ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2015/2020, kwahiyo Shule ya Sekondari NKUMBA ndiyo naanza nayo’’ alisema Komanya.
Aidha Komanya alitumia fulsa hiyo kuwaagiza Wakuu wa Shule zote zilizopo Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanapanda miti kwenye maeneo yote ya shule zao kuonyesha mipaka ya shule, kwa kufanya hivyo kutasiadia sana kuzuia wavamizi wa maeneo ya shule na kuepuka migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima.
Pia akamugiza Afisa Elimu Sekondari Manispaa ndugu Chatta Luleka kuhakikisha anapeleka wataalamu wa ardhi ili wapime na kuainisha ukubwa halisi wa maeneo ya shule hizo mbili kabla ya kuanza kujengwa hayo madarasa.
Kwa upande wake Chatta Luleka amabae ndiye Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Tabora, alimshukuru sana Mkuu wa Wilaya kwa namna ambavyo amekuwa na maono yenye tija na afya sana kwa wakazi wa Manispaa ya Tabora hasa kwakuwa amekuwa mbunifu na msimamizi mzuri sana kwenye kuinua Elimu kwa Manispaa ya Tabora. Na akamuahidi kutekeleza maagizo yote anayoyatoa ili kuifanya Manispaa ya Tabora inakuwa bora zaidi kuliko wakati wowote.
Kuanzishwa kwa kidato cha tano na sita katika shule hizo za NKUMBA na CHANG’A kutakuwa ni mkombozi sana kielimu kwakuwa hapakuwahi kuwa na High School tangu kuazishwa kwa shule hizo. Ambapo Shule ya Sekondari Chang’a kutakuwa na michepuo miwili ya HGL na HKL, wakati Shule ya Sekondari Nkumba itakuwa na michepuo ya PCB na CBG, na ukizingatia kuwa wanafunzi wamekuwa wakienda umbali mrefu kufuata elimu hasa ya kidato cha tano na sita.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.