Kundi la mawasiliano kwa njia ya mtandao la walimu wa Shule za Msingi za Manispaa ya Tabora (WhatsApp Group) limekabidhi bidhaa mbalimbali kwa Kituo cha Kulelea watoto yatima cha Igambilo.
Vitu hivyo ambao vina thamani ya zaidi ya shilingi laki nane ambavyo ni pamoja na Mchele, sukari, maharage, mafuta ya kupikia, nyama, chumvi, soksi, vyandarua, taulo za kike, sabuni, dafatri, vichongeo, vifutio, kalamu,juisi na biskuti.
Akikabidhi msaada huo kwa Mlezi na Mwalimu wa Kituo hicho kwa niaba ya walimu hao, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Tabora Bw. Joel Mkuchika alisema kuwa wanatoa msaada huo ili watoto hao nao wajione kama sehemu ya jamii na waweze kutimiza ndoto zao ikiwemo za kupata elimu bila vikwazo.
Alisema kuwa ni vema walimu na wanajamii wakaendelea kujitolea kwa watoto kama hao ambao wanahitaji msaada wakati wote ukizingatia kuwa hawana wazazi isipokuwa wazazi wao ni jamii inayowazunguka.
Mkuchika alisema ni vizuri jamii ikajiwekea utaratibu kuwafikia watoto hao na wengine wenye hali kama hii na kuwasaidia kwa kadiri itakavyowezakana ili nao hapo baadae waweze kushiriki katika ujenzi wa Taifa katika sekta mbalimbali kama watumishi na wataalamu.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kila tarehe 16 Juni kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Haki za Mtoto Kwanza’.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.