Na Alex Siriyako:
Walimu 1680 ambao ni jumla ya walimu wote wa shule za msingi na Sekondari katika Manispaa ya Tabora wamepata Vishikwambi ambavyo vimetolewa na Serikali kwa ajili ya kulahisisha zoezi la kufundishia na Ujifunzaji kwa Waalimu hao. Zoezi la kugawa Vishikwambi hivi limefanyika leo Januari 24, 2023 katika Shule ya Sekondari Kazima iliyopo Tabora Mjini.
Mhe. Ramadhani Kapela,ambae ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora akigawa Vishikwambi hivi kwa Walimu amewaasa wakavitunze, wavitumie kwa kazi halisi iliyokusudiwa na anaamini kwa mwaka huu wa masomo kutakuwa na matokeo chanya kwa mitihani inayokuja kwani Walimu hawatokuwa na uhaba wa Vitabu tena kwa maana Maktaba Mtandao kupitia Vishikwambi hivi inamaliza uhaba huo. Hivyo amewataka Walimu wakafanye kazi kwa weledi na jitihada Zaidi.
Aidha Mhe. Kapela ameongeza kuwa Serikali haitosita kumchulia hatua ikiwa ni pamoja na kulipa Kishikwambi, Mwalimu yeyote ambaye kwa uzembe wake ataharibu Kishikwambi hicho ama kukipoteza. Amesema sio kila Mwalimu ni mwaminifu sana na Serikali inatambua hilo, hivyo Manispaa kupitia Idara ya Elimu Sekondari na Msingi itaweka utaratibu wa kuvifuatilia Vishikwambi hivyo na kuhakikisha kama viko salama na vinaendelea kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na Serikali.
Nae Mwalimu Fortunata Muyaga ambae ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Uhuru ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassani kwa kuwapatia Walimu Vishikwambi hivyo kwaajili ya kuongeza ufanisi katika kazi nzima ya ufundishaji mashuleni na ameahidi kwa niaba ya Walimu wenzie kuvitunza Vishikwambi hivyo na kuleta matokeo chanya kwa sababu uhaba wa vitabu hautokuwepo tena na hata mfumo wa uandaaji wa vipindi na utunzaji wa taarifa umerahisishwa.
Katika Kuhitimisha zoezi hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndugu Sefu Salum Sefu amemshukuru Mstahiki Meya kwa kukubali wito wa kuja kugawa Vishikwambi hivi kwa Walimu. Lakini pia amemshukuru Rais Samia kwa jitihada zake kubwa za kuboresha Sekta ya Elimu Nchini mathalani ujenzi mkubwa wa miundombinu na upatikanaji wa Vishikwambi hivyo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.