Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt Batilda Buriani leo tarehe 22.6.2021 amewaapisha wakuu wa Wilaya wapya wawili ambao ni Dkt Yahya Nawanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini na Ndg. Matiko Paul Chacha
Hafla hiyo imefanyika kwenye Ukumbi wa Mtemi Mwanakiyungi uliopo kwenye jengo la Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambapo Mhe Buriani alitumia fulsa hiyo kujitambulisha rasmi mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Viongozi mbalimbali wa kiserikali, kidini, taasisi, Wakuu wa Idara, Vitengo, waandishi wa habari na wadau baada ya kuwa ameteuliwa kushika nafasi ya Mkuu wa Mkoa akitokea Mkoa wa Shinyanga ambako alikuwa akihudumu kama Katibu Tawala wa Mkoa.
Katika hotuba yake Dkt. Buriani amewataka Wakuu wa Wilaya kwenda kuwa Viongozi wa kwenye maeneo yao na siyo kwenda kuwa watawala huku akisistiza uwajibikaji wenye kuzingatia sheria, kanuni, miongozo mbalimbali huku wakimtanguliza Mungu kwenye majukumu yao.
Dkt. Buriani pia akawataka kwenda kushirikiana vema na Wakurugenzi kwenye Halmashauri zao ili waweze kumsaidia Mhe. Rais hasa kupunguza kero kwa wananchi pamoja na kuboresha huduma kwa jamii wanazoziongoza.
“Nawasihi Wakuu wa Wilaya wote kuwa, muende kuwa Viongozi kwenye maeneo yenu na siyo kuwa Watawala, huku mkiwajibika kwa uwazi, ukweli na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo na mkashirikiane vema na Wakurugenzi wenu vizuri ilituweze kumsaidia Mhe Rais wetu kuleta hudma bora kwa wananchi wetu,” alisisitiza Dkt Buriani.
Aidha kwenye hotuba yake aliweza kubainisha baadhi ya vipaumbele vyake ikiwamo; Ulinzi na Usalama, Ukusanyaji wa mapato, Afya, Elimu,Kusimamia miradi ya maendeleo, Utunzaji wa mazingira, Kutatua kero za ardhi na mirathi.
Sambamba na hayo, Mhe Dkt Buriani alisisitiza kuwa atasimamia na kufuatilia kwa karibu zaidi suala la Ufaulu kwa ngazi zote za elimu ya msingi na sekondari, Bima ya Afya, pesa ya asilimia kumi kwa kila Halmashauri zinazotengwa kwa ajili ya makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Asilimia inayotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kila Halmashauri.
Pia kuboresha michezo mashuleni, pamoja na suala la hati chafu kwa Halmashauri kwamba lisijirudie tena huku akiwataka Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kutenga angalau siku moja kwa kila wiki ili waende kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zao, na kwamba wakuu wa Idara na Vitengo pia wasikae maofisini, na badala yake watoke kwenda kwa wananchi kutatua kero zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mheshimiwa Dkt. Yahya Ismail Nawanda, alimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumjalia uzima, pia akamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu kwakuwekeza imani kwake na hata akamteuwa kuwa kwenye nafasi hiyo ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora.
Nakwamba alimuahidi Mheshimiwa Rais, Mama Samia pamoja na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt Buriani kwamba atafanya kazi kwa weredi wake wote, kwa kujituma, na kwa kushirikiana na wenyeji aliowakuta ili kuifanya Wilaya ya Tabora isonge mbele kimaendeleo na hatimae kufikia malengo ya wana Tabora na Taifa kwa ujumla.
“Mimi siyo mjuzi wa kila kitu, nimekuja Tabora ili tushirikiane sote, tuijenge sote ili tumsaidie Mhe. Rais hasa kutatua matatizo ya wananchi, hivyo basi kufanikiwa kwangu kunategemea sana ninyi wenyeji wangu katika kutekeleza majukumu yangu”, alisema Dkt. Nawanda.
Uapisho huu wa Wakuu wa Wilaya unafuatia baada ya Mhe. Rais kufanya baadhi ya mabadiliko ya wateule wake wakiwamo Wakuu wa Wilaya na Mikoa siku za hivi karibuni hasa kwa Wakuu wa Wilaya mabadiliko yalifanyika tarehe 19.6.2021 na Wilaya ya Tabora akateuliwa Mhe. Dkt. Yahya Ismail Nawanda.
MWISHO.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.