Na Paul Kasembo.
Waheshimiwa Madiwani kutoka Manispaa ya Tabora walifanya ziara ya siku mbili kwa ajili ya kujifunza namna bora na njia sahihi zenye lengo la kuongeza Ukusanyaji wa Mapato, kuona namna Miradi Mikubwa ya Kiuchumi na Uwezeshaji wa Viwanda katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama.
Akizungumza wakati wa ukaribisho wa ziara hiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama Mhe. Sindano Machumu aliwaeleza Waheshimiwa Madiwani kutoka Manispaa ya Tabora wawe huru kuuliza, kuhoji, kukosoa kushauri na kutoa mapendekezo yoyote kwa kadiri watakavyokuwa wameona kwenye ziara hiyo, ikiwa ni sehemu yao pia Kahama kujisahihisha na kujiweka veama zaidi.
“Pamoja na kwamba hapa Kahama tumekuwa tukipokea ugeni mwingi wenye dhamira ya kuja kujifunza mambo mbalimbali, lakini kwa Manispaa ya Tabora tunafurahia zaidi ujio wenu kwani ni jirani zatu, ndugu zetu na wamoja katika kuhudumia jamii zetu amabzo zimepakana, hivyo muwe huru zaidi na tupo tayari kupokea maoni yenu na kuyafanyia kazi tukijuwa nasi tutakuja kujifunza kwenu pia”, Mhe. Machumu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Ndg Anderson Msumba, alimshukuru sana Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela kwa kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani kuichagua Kahama kuwa sehemu ya mafunzo yao, kwakuwa anaamini kuwa ziara hiyo itakuwa na tija kubwa kwao na kwa wananchi wao kwa muktadha mpana wa Manispaa ya Tabora, kisha akawakata kushiriki kikamilifu sasa kwenye ziara.
Pamoja na salamu hizo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama alipata wasaa wa kuelezea namna ambavyo wanatekeleza ukusanyaji wa mapato,uendeshaji wa miradi mikubwa na uwekezaji wa viwanda.
Manispaa ya Kahama imeweza kupiga hatua kubwa sana kwenye kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kuwawezesha kimiundombinu wafanyabiara wadogowadogo (CDT) kwa kuwatengenezea maeneo ya kibiashara bure ikiwa ni pamoja na kuanzisha kituo kidogo cha mabasi, kujenga mabanda ya wauza mitumba.
Kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya barabara, umeme, maji na mitaro, na kisha kufanya maboresho kwa makubaliano na na wafanyabiashara hao ambao wanaendelea na ujenzi wa vibanda vya biashara kwa uataratibu wa JENGA, TUMIA HAMISHA (Build, Operate and Transfer) gaharama ambazo zinafanywa na mfanyabiarasha mwenyewe baada ya kuwa amewezeshwa na Manispaa kama ilivyoelezwa awali.
”Kwa kufanya hivi peke yake, Kahama inaweza sasa kukusanya mapato yake kwa wingi zaidi kwakuwa imewawezesha wafanyabiashara hao na wao hulipa bila hata tatizo tena kwa wakati bila shuruti yoyote”, alisema Anderson.
Kwa upande wa Miradi Mikubwa ya Kiuchumi na Viwanda, wametenga eneo maalumu (CHAPULWA) ambalo lipo pembezoni kabisa mwa Manispaa ya Kahama, likapimwa, likapatiwa HATI, kulipwa fidia wananchi wa eneo hilo na kisha kuwapatia wawekezaji wakubwa bure kabisa lenye ukubwa wa hekari mia saba.
Kisha Manispaa ikawezesha kupeleka miundombinu yote muhimu ikiwamo, barabara, maji, na baadae wanamalizia na nishati ya umeme, jambo ambalo limewezesha kupatikana kwa wawekezaji wakubwa wa viwanda vya usindikaji mafuta ya kula, utengenezaji wa mabati, mabomba ya maji, uunganishaji wa pikipiki nk.
“Hiyo peke yake kwa kuanzia kunaiwezesha Manispaa ya Kahama kukusanya Service Levy ya kutosha, kuongeza ajira kwa wananchi wa Kahama, kuboresha maisha kiuchumi, kuongeza mzunguuko wafedha ambapo sasa wanakusanya takribani asilimia 16.1 ya bajeti yote ya Manispaa ya Kahama”, alisisitiza Anderson.
Miradi mingine mikubwa ni uanzishwaji wa Eneo la Uwekezaji Mwendakulima, eneo hilo lina ukubwa wa ekari 170, lipo umbali wa kilomita 6.3 kutoka katikati ya Mji wa Kahama ambapo wanaendesha shughuri za usafirishaji wa mizigo kwenda Tinde, Lusumo, Burundi, DRC Congo, Uganda na Sudani Kusini pamoja na kuanzisha Hotel na Shopping Mall.
Sambamba na hayo pia wanatarajia kuanzisha Soko la Kimataifa la Mazao Busoka am,bapo kutakuwa namashine kubwa za kisasa za kuchambua, kufunga na nafaka na mbogamboga ambapo wapo hatua ya upembuzi. Lengo la mradi huu mkubwa kuwezesha ununuzi wa mazao ya kilimo hasa nafaka mchele/mahindi kwa kujenga soko la ndani na nje hususani nchi za Mzaiwa Makuu na Sudani Kusini.
Ambapo wataweza kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, pato la Manispaa, kutoa ajira zaidi ya 6,000, kuwa na soko la uhakika kwa wananchi wao na kuchochea maendeleo ya Sekta zingine.
Akihitimisha ziara hiyo ya siku mbili, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda aliwapongeza sana Kahama kwa juhudi zao na maarifa wanayoyatumia kufanisha shughri za maendeleo, akawashukuru sana kwa ukarimu na ushirikiano waliuwapatia Waheshimiwa Madiwani na kwamba watakwenda kuyatekeleza yote waliyoyaona na kujifunza kutoka Kahama, na mwisho aliwakaribisha Manispaa ya Tabora na wao waje kujifunza.
Kukamilika kwa ziara hii ya siku mbili katika Manispaa ya Kahama kutaleta tija kubwa sana kwenye utekelezaji wa malengo ya Manispaa ya Tabora wenye dhamira ya kuipaisha kiuchumi, kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwawezesha na kuongeza mapato kwa ujumla.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.