Na Alex Siriyako,
Wafanyabiashara na Wajasiriamali walioko Manispaa ya Tabora na Tanzania kwa ujumla wamehimizwa kuwekeza kwenye fursa za kiuchumi zinazopatikana katika Manispaa ya Tabora. Miongoni mwa fursa za kiuchumi zilizoainishwa ni pamoja na Uwekezaji kwenye Viwanda vikubwa na vidogo, Ujenzi wa Hotel za Kisasa pamoja na Uwekezaji kwenye sekta ya Elimu na afya.
Ujumbe na hamasa hizi zimetolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Kapela, akimuwakilisha Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Paul Chacha katika Baraza la Biashara Manispaa ya Tabora. Baraza hili kimsingi huwakutanisha Sikta Binafsi na Sekta ya Umma na kujadili kwa Kina changamoto na fursa zilizopo na kuzipatia ufumbuzi ili kuharakisha maendeleo ya Watanzania.
Katika Baraza hili ambalo limefanyika ukumbi wa Manispaa ya Tabora, baadhi ya Changamoto zimebainishwa mathalani uhaba wa miundombinu kwenye masoko, uchakavu wa miundombinu kwenye machinjio ya Tabora, Bajaji na Bodaboda kutokuwa na vituo maalumu hivyo kuleta usumbufu kwa wateja, Wazabuni wa usafi kutowajibika ipasavyo pamoja na mikopo ya asilimia kumi kutotosheleza mahutahi ya walengwa.
Mhe. Ramadhan Kapela ametoa ufafanuzi na maagizo kwa Menejimenti ya Manispaa ya Tabora katika kupata ufumbuzi wa changamoto hizo, miongoni mwa maagizo hayo ni pamoja na Watendaji Kata kusimamia ipasavyo Vikundi vya usafi na kukusanya ushuru wa taka ngumu, Jengo la Machinjio likarabatiwe ndani ya mwaka huu wa fedha, na amemtaka Afisa Biashara kuhakikisha miundombinu yote kwenye masoko inafanya kazi.
Aidha Bwana Festo Nashoni, Afisa Biashara wa Manispaa ya Tabora kwa nafasi yake ameeleza kwa kina fursa za uwekezaji katika Manispaa ya Tabora, fursa hizo zikiwa ni pamoja na uwekezaji wa Viwanda vikubwa na Vidogo, Ujenzi wa Hotel na Nyumba za kulala wageni na hii ikichangiwa na ongezeko la wageni wengi kutokana na ujenzi wa Miradi ya Kitaifa ya kimkakati kama Reli ya Kisasa kutoka Makutupora-Singida hadi Tabora.
Bwana Nashoni amedadavua kuwa Manispaa inatarajia vilevile kuwa na Miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa Karakana ya reli ya mwendo kasi, ujenzi wa soko kuu la kisasa, ujenzi wa stendi kubwa ya mabasi , ujenzi wa Kitega Uchumi cha Halmashauri (ppp) pamoja na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Teknolojia na Kilimo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Aidha katika kuhitimisha, Wajumbe wa Baraza la Biashara waliomba Serikali ione namna ya kuipa Manispaa ya Tabora mahindi kutoka ghara la Taifa ili kupunguza kasi ya njaa kama ambavyo miji mingine imepewa mahindi hayo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.