Vijana waendesha bajaji na bodaboda katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wamefanya maandamano ya AMANI na kujitolea jumla ya chupa 38 za damu ili kuokoa maisha ya majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro.
Akiongea Mwenyekiti wa Chama Cha Waendesha Bajaji Manispaa Bw Said Maganga alisema kuwa wamejitolea kiasi hicho cha damu ili kusaidia majeruhi waotekwenye ajali hiyo ambao wamelazwa hospitalini.
‘Tumeguswa sana, sana na tukio hilo hasa ikizingatia kwamba miongoni mwa majeruhi na waliopoteza maisha ni vijana wenzetu waliokuwa
wanaotoa huduma ya usafiri wa bajaji na bodaboda katika eneo hilo laMsamvu, Mkoani Morogoro’ alisema Maganga.
Aidha Maganga alisema kuwa msiba huo ni wa Kitaifa kwani baadhi ya majeruhi na wale waliopoteza maisha walienda pale kwa ajili ya kutoa msaada kwa
wenzao lakini kwa bahati mbaya nao wakaunguzwa na moto huo.
‘Tunaomba Mwenyezi Mungu aziweke mahali pema peponi roho za marehemu wote na wale wote waliojeruhiwa awafanyie wepesi wapone kwa haraka…’ Maganga alisema.
Akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema kuwa ajali za barabarani zinaepukika, hivyo akawataka waendesha bajaji na bodaboda kuwa makini wanapokuwa barabarani na vyombo vya moto.
Aliwahusia waendesha vyombo vya moto na jamii wote kwa ujumla wanayo fursa kubwa ya kulinda maisha yao kama kila mmoja atakuwa makini barabarani na kufuata sheria za usalama barabarani.
Pamoja na yote hayo lakini pia alionya tabia ya baadhi ya madereva wa vyombo vya moto ikiwemo waendesha bajaji na bodaboda kuongea na simu wakati wanaendesha hivyo akawataka kuacha mara moja tabia hiyo.
Nae Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula akitoa salamu za Kitaifa wakati akiwa kwenye ziara mkoani Tabora alisema kuwa, alisema kuwa anawapongeza sana vijana wote walioguswa na tukio hilo na kwa moyo wao wa uzalendo na kuwaunga mkono kwa kuchangia damu.
Aliwataka wanajamii wote kujiwekea utamaduni wa kukwepa majanga ya moto na kutoshabikia mambo yoyote yanayoweza kuhatarisha maisha yao, aidha
aliwataka Jeshi la Polisi na Zimamoto kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na majanga ya moto kwa jamii wakati wote ili wananchi wapate uelewa wa namna ya kujikinga.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.