Na Alex Siriyako,
Manispaa ya Tabora ikiwa ni miongoni mwa Halmashauri zilizopo Nchini imezindua rasmi Miongozo na mikakati ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji ngazi ya Elimu Msingi na Sekondari. Uzinduzi huu umeshuhudiwa na wageni na Viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu wakuu wa Shule za Msingi, Waratibu Elimu Kata, Wathibiti Ubora wa Shule, Maafisa Elimu, Madiwani , Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Maiga Nyanja pamoja na Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapera.
Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikikabiliana na changamoto nyingi sana zinazowasibu Watanzania. Sekta ya Elimu nayo ni miongoni mwa Sekta zenye Changamoto nyingi sana na hivyo kuilazimu Serikali kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo ambazo ni pamoja na Uhaba wa Madarasa, uhaba wa Madawati, Upungufu wa Walimu pamoja na Vifaa vya kujifunzia.
Ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathimini ya mara kwa mara ili kuona maendeleo ya Elimu ya Msingi na Sekondari. Tathimini ya hivi karibuni imebaini uwepo wa mafanikio makubwa lakini pia baadhi ya Changamoto, hii ikiwa ni kutokana na Uwekezaji Mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya sita kwenye Sekta hii hususani kumaliza uhaba wa madarasa, uhaba wa Walimu na uhaba wa Madawati.
Aidha Ofisi ya Rais –TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu katika kukabiliana na Changamoto zinazoikabili Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari Nchini, Imeandaa Zana kuu tatu za kuzingatiwa katika usimamizi na uendeshaji wa shule;
Mgeni Rasmi katika hafla hii ambaye ni Mustahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapera amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassani kwa upendeleo mkubwa sana kwa manispaa ya Tabora hususani Sekta ya Elimu na kipekee sana amemshukuru Mhe. Rais kwa fedha zilizokuja hivi karibuni kwa ajili ya kujenga madarasa fedha zaidi ya bilioni moja milioni miatatu.
Mustahiki Meya amewapongeza Walimu wa Manispaa ya Tabora kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhakikisha Wanafunzi wanafaulu vizuri lakini vilevile pongezi hizo zikaenda sambamba na usimamizi mzuri wa Miradi ya Maendeleo kwa fedha zinazoletwa na Serikali Mashuleni.
Mhe. Ramadhani Kapera ametanabaisha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora katika mwaka wa fedha unaokuja, Manispaa itaweka kipaumbele zaidi ujenzi wa Nyumba za Walimu na Manesi kwani kundi hili la Watumishi ni nyeti na ni kundi lenye watumishi wengi na linafaa kupewa kipaumbele sana kulingana na umuhimu wake mkubwa.
Aidha Mhe. Kapera amewasihi na kuwataka Wakazi wa Tabora wabadilike waweke elimu kuwa kipaumbele kwao. Amewataka watoe ushirikiano mkubwa kuhakikisha kuwa watoto wanakula chakula shuleni kwani shibe ni miongoni mwa sababu zinazochangia ufaulu kwa watoto. Hata hivyo amewataka Walimu na Waratibu Elimu Kata wasichoke kuwaelimisha Wananchi na kuendelea kuwahamasisha kuchangia chakula ili Manispaa iweze kuongeza ufaulu katika mitihani ya Kitaifa.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Dkt. Peter M. Nyanja amewataka Wakuu wa Shule watoe Matangazo kwa Umma mara wapatapo fedha za Miradi ili Jamii nayo ishiriki vyema kwenye kujenga na kusimamia matumizi sahihi ya fedha hizo, lakini villevile jamii iweze kutambua ni kwa kiasi na kasi ipi Serikali ya Awamu ya Sita inaleta pesa kwenye miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Aidha Dkt.Nyanja ametumia fursa hii kuwaeleza Wakuu wa Shule kuwa kwa sasa kwa Shule zenye Miradi,kabla Mkuu wa Shule hajaandika Muhtasari wa malipo analazimika kuwasiliana na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji ya Manispaa ili aweze kufika kwenye mradi husika na timu yake na kukagua kama ubora umezingatiwa kwenye mradi ikiwa sambamba na taratibu zote za Manunuzi kama zimefuatwa ndipo malipo yaendelea.
Aidha, Bi.Haika Masue, akimwakilisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imejipanga vyema sana kwaajili ya ufuatiliaji na Usimamizi wa fedha zote za Serikali zinazokwenda kwenye miradi ya maendeleo katika Sekta zote ndani ya Manispaa ya Tabora.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.