Na Alex Siriyako:
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia zaidi ya asilimia mia moja na nane katika kujenga miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Serikali Kuu ilitenga bajeti ya maendeleo ya bilioni kumi na mbili (12) katika Manispaa ya Tabora kwa mwaka huo wa fedha, na ikaleta bilioni kumi na tatu (13) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia zaidi ya nane.
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imetumia zaidi ya bilioni mbili kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka kwenye mapato yake ya ndani, huku wafadhiri nao wakitoa zaidi ya milioni mia nane ambazo kimsingi ni kiwango cha chini ya ahadi zao.
Serikali Kuu imevunja rekodi yake yenyewe kwa kuleta fedha za miradi ya maendeleo kwa zaidi ya asilimia mia moja hasa kwa miaka ya hivi karibuni.
Taarifa hii ya mwaka wa fedha 2023/2024 imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndugu Elias M. Kayandabila leo Agosti 14,2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kufunga mwaka wa fedha 2023/2024, kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora.
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, wameishukuru sana Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuipendelea Manispaa ya Tabora kwa miradi mingi sana ya maendeleo katika sekta za Afya, Elimu, Kilimo na Mifugo, pamoja na Miundombinu ya Barabara.
Aidha, katika Baraza hili la kumaliza mwaka wa fedha 2023/2024, wajumbe wa baraza wamefanya uchaguzi wa kumpata Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora pamoja na wenyeviti wa Kamati za Kudumu kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo Mhe. Adam Kalongo, Diwani wa Kata ya Kabila kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) ameibuka mshindi wa kiti cha Naibu Meya.
Aidha Mhe. Zinduna Kisamba, Diwani wa kata ya Tambukareli (CCM) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti kamati ya Maadili, Mhe. Elias Ndelemba, Diwani wa Kata ya Tumbi (CCM) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mipangomiji, Ujenzi na Mazingira, Mhe. Paulo Kananda, Diwani wa Kata ya Mbugani(CCM) amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Kapela ameishukuru sana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi kemkem ya maendeleo, aidha ameendelea kuipongeza Manispaa ya Tabora kwa kukusanya mapato kwa asilimia mia moja mwaka wa fedha 2023/2024, lakini pia amewashukuru Madiwani kwa uchaguzi mzuri, na zaidi ya yote, amewapongeza viongozi waliomaliza muda wao na waliochaguliwa kushika nafasi hizo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.