Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt.Phillemon Sengati amezindua rasmi Baraza la Madiwani la Manispaa ya Tabora huku akiwataka kusimamia na kudhibiti matumizi ya fedha za umma ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuwasaidia ya kupeleka maendeleo kwa wananchi wa Manispaa ya Tabora.
Alisema fedha zote ni lazima zitumike kwa kuzingatia mipango na bajeti za Halmashauri na Serikali kwa ujumla kupitia Sheria ya Bajeti na ile ya fedha za umma.
Dkt. Sengati alitoa kauli hiyo leo wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, baraza amabalo limeketi kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2020 ambapo awali lilitanguliwa na uchaguzi wa Naibu Mstahiki Meya, Meya pamoja Wenyeviti wa Kamati za Kudumu.
Alisema Madiwani wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa fedha zote zinazoletwa na Serikali kuu na zile walizokusanya zinatumika kwa usahihi na uwazi na kuzipeleka katika shughuli mbalimbali za wananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema hatua hiyo itasaidia kuepuka matumizi yasiyokuwemo katika bajeti waliyopitisha ambayo yanarudisha nyuma maendeleo na kuwasononesha wananchi.
Dkt. Sengati alisema ili kudhibiti ufujaji wa makusanyo ya Halmashauri ni lazima fedha zote zikusanywe kwa kutumia mashine (POS) na kutoa stakabadhi kwa waliotoa fedha.
Aidha Dkt Sengati alipiga marufuku kwa watendaji waliopewa dhamana ya kukusanya mapato kutumia vitabu kuandika kwa mkono wakati wa makusanyo ya mapato ya Halmashauri kwa kuwa njia hiyo ndio inayotumika kuiba fedha za umma kwa kutoa taarifa zisizostahili za ukusanyaji wa fedha.
Mkuu huyo wa Mkoa aliongeza kuwa Madiwani wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna fedha inayotumika kabla ya kupelekwa benki.
Alisema utumiaji wa fedha ambazo hazipita Benki (fedha mbichi) unasababisha kuzalishwa kwa hoja za kiugazi na wakati watendaji wasio waadilifu kutumia nafasi hiyo kuiba fedha za umma.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka Madiwani kuhakikisha wanasimamia na kuwahimiza watendaji katika maeneo yao kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuiwezesha Manispaa ya Tabora kuwa na fedha nyingi zitakasaidia katika shughuli za maendeleo ya wananchi.
Alisema ni lazima wajipange kuhakiksha kuwa ifikapo mwaka 2025 wanakuwa na mapato ambayo watakuwa tena hawategemei fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu.
Katika hatua nyingine Madiwani wa Manispaa ya Tabora wamemchagua Diwani wa Kata ya Isevya Mhe. Ramadhani Shabani Kapela kuwa Mstahiki Meya, aidha Baraza lilimchagua Diwani wa Kata ya Chemchem Mhe. Alhaj Kasongo Amrani kuwa Naibu Meya.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.