Na Alex Siriyako:
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt.Batilda Buriani amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora kutenga fedha kwaajili ya Sekta ya ardhi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Dkt. Batilda ametoa maagizo haya leo Machi 6,2024 katika ukumbu wa Chuo cha Uhadhili ambapo alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa Wadau kujadili utekelezaji mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unaoenda kwa kauli mbiu isemayo Usawa wa Kijinsia katika Umiliki wa Ardhi kwa Ustawi wa Jamii.
Dkt. Batilda amesisitiza kuwa bajeti hiyo itakayotengwa ni kwaajili ya kuendeleza maeneo yote ambayo hayataguswa na mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika Halmashauri hizo za Mkoa wa Tabora.
Mradi wa LTIP ni mradi ambao unatekelezwa na Serikali chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Malengo mahsusi ya mradi huu ni mwendelezo wa kuhakikisha Wananchi wa mjini na vijijini wanakuwa na umiliki rasmi wa ardhi yao hasa iliyopimwa kitaalamu.
Kwa Mkoa wa Tabora mradi huu utatekelezwa katika Halmashauri za Kaliua, Sikonge, Uyui, Urambo, Nzega Mjini, Nzega Vijijini na Manispaa ya Tabora.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa LTIP Bw.Joseph Shewiyo amesema mradi huo unalenga kupanga matumizi bora ya ardhi kwa maendeleo ya vijiji na miji, kuhamasisha umiliki wa ardhi kwa pamoja, kuzingatia haki za makundi maalumu katika umiliki wa ardhi pamoja na usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi.
Bwana Shewiyo ameongeza kuwa hadi sasa mradi huu umeongeza idadi ya wanawake wanaomiliki ardhi kutoka asilimia 25 hadi 38, hali inayosaidia kufikia azima ya Serikali ya kuwaletea Wananchi usawa wa kijinsia katika umiliki wa ardhi.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.