Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Phillemon Sengati amekabidhi hundi yenye thamani shilingi milioni 142 kwa vikundi 29 vya wanawake na vijana wa Manispaa ya Tabora.
Mikopo hiyo imetolewa kwa vikundi hivyo ikiwa ni sehemu ya Manispaa ya Tabora kutimiza takwa la Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2019 inayoitaka kila Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu.
Dkt. Sengati amekabidhi mikopo hiyo katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa jengo la Manispaa lilipo Viwanja vya Nane Nane maarufu kwa jina VIwanja vya Fatuma Mwasa.
Akikabidhi mfano wa hundi hiyo, Dkt. Sengati alivitaka vikundi vilivyopata mkopo kutumia fedha hizo katika miradi na malengo waliyoombea mikopo na sio katika shughuli nyingine zisizokuwa za maendeleo.
“Nendeni mkazitumie pesa mlizozipata leo kwenye miradi, malengo na makusudio ya mikopo yenu kama ambavyo amliomba na wala msiende kuzitumia kinyume na kusudio la shughuli zisizokuwa za kimaendeleo, ili ifike wakati muweze kusafirisha biashara zenu nje ya Mkoa na hata mpaka nje ya Nchi,” alisema Dkt. Sengati.
Aidha Dkt. Sengati aliutaka Uongozi wa Manispaa kuandaa mpango wa kutoa elimu ya Usimamizi wa Fedha na kufikiri kimkakati kwa wajasiriamali kabla ya kuwapa mikopo ili waweze kutumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao wenyewe, na Taifa kwa ujumla.
Sanjari na hayo, Dkt Sengati aliutaka uongozi wa Manispaa ya Tabora kutoa mikopo kwa uwazi bila ucheleweshaji na kuepuka rushwa kwa vikundi vinavyoomba na kwamba ifike wakati sasa uongozi wa Manispaa utoe fedha nyingi na vifaa kwa vikundi ili matokeo yake yaweze kuleta tija kwao wenyewe na Mkoa kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Christina Bunini alisema katika mwaka wa fedha unaoendelea wametenga kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 445 kwa ajili mikopo ya vikundi kama sheria inavyotaka.
Alisema kati ya fedha hizo wamepanga kutoa kiasi cha shilingi milioni 178 kwa wanawake, milioni 178 kwa vijana na milioni 89 kwa watu wenye ulemavu.
Bunini aliongeza hadi hivi wameshapokea maombi mengi zaidi ya fedha ya fedha iliyotengwa katika bajeti.
Alisema toka Julai hadi Oktoba mwaka huu wameshapokea maombi ya mikopo kwa vikundi 79 ambayo thamani yake ni sawa na shilingi milioni 566.5.
Bunini alisema kati ya fedha hizo vikundi 61 vya wanawake vimeomba kiasi cha shilingi milioni 463, vijana 12 vimeomba shilingi 76 na watu wenye ulemavu 6 vimeomba shilingi milioni 27.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Tabora Tumaini Mgaya alisema hadi hivi sasa Manispaa ya Tabora imekwisha kutoa kiasi cha shilingi milioni 211 kwa vikundi 41.
Alisema kuwa pamoja na jitihada hizo kuna baadhi ya vikundi vimekuwa havirejeshi mikopo kwa wakati na kusababisha wanavikundi wengine wanaohitaji kuchelewa kupata fedha.
Alisema miongoni mwa vikundi ambavyo vinadaiwa ni vya vijana na watu wenye ulemavu na kuna baadhi ya vikundi vimekuwa vikianzisha miradi tofauti na ile waliyombea mikopo
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.