Na Alex Siriyako,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amepata fursa ya kuzungumza na Wakazi wa Mkoa wa Tabora katika uwanja wa Ally-Hassan Mwinyi uliopo Manispaa ya Tabora Mkoani Tabora. Mhe. Rais amewahutubia Watanzania kupitia hadhara hiyo ikiwa ni hotuba ya kuhitimisha ziara yake ya Kikazi ya siku tatu mfululizo Mkoani Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Buriani katika kuwasilisha salamu za Wananchi wa Tabora amemshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali wito wa kuja kuwatembelea Wakazi wa Tabora na kuwasikiliza baadhi ya changamoto zao. Lakin kubwa amemshukuru sana Mhe.Rais kwa fedha nyingi sana kwenye miradi mbalimbali ambapo zaidi ya bilioni 46 zimetumika sekta ya Elimu zaidi ya bilioni 29 zimetumika TARURA na zaidi ya Bilioni 25 zimetumika sekta ya maji. Hivyo kwa niaba ya Wanatabora amemshukuru sana Rais.
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa, akimkaribisha Mama kuongea na Wananchi wa Tabora amesema kwamba Wizara yake imetenga zaidi ya Tirilioni nane kwa ajili ya miradi katika na amepokea changamoto zote za Wabunge katika maeneo yao na ameahidi kuzifanyia kazi na zaidi ya yote Wizara yake imeongeza bajeti ya usimamizi wa miradi kwa ngazi za Wilaya na Mikoa.
Mhe. Rais Katika Ziara ndani ya Mkoa wa Tabora ameweza kufungua rasmi barabara za Nyahua –Chaya yenye urefu wa Km 85.4, Barabara ya Tabora-Koga yenye urefu wa Km 342 pamoja na kukagua miradi ya maendeleo mbalimbali inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Tabora.
Mhe. Samia Suluhu amewashukuru sana Wananchi, Wakuu wa Wilaya, Machifu pamoja na Viongozi wa Dini wa Mkoa wa Tabora kwa mapokezi mazuri na zaidi kwa kipindi chote alichokaa hapa Tabora.
Mhe. Rais amewataka sana Wanachi wa Tabora walinde Miondombinu ambayo wanaipata kwani sio kila Mkoa unapata fursa hizi. Miongoni mwa miondombinu hiyo ni pamoja na Barabara za lami, Alama za barabarani, Taa za barabarani, Miundombinu ya Reli pamoja na miundombinu ya Maji. Vilevile amewataka Wanatabora kuchangamkia fursa za ajira zilizopo kutokana na ajira zitokanazo na miradi inayoendelea kama SGR pamoja na ujenzi wa miradi mingine.
Mhe. Rais amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kuleta maendeleo Tabora na maeneo mengine ya Nchi kulingana na vipaumbele vilivyopo kwenye ILANI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni sambamba na malengo ya Dunia ya kuleta maendeleo ya Kijani (SDGs).
Mhe. Samia ametanabaisha kwamba mwaka ujao wa fedha kipaumbele kikubwa cha Serikali ni Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kwani ndio Sekta zinazogusa kundi kubwa la Watanzania, hivyo Serikali imeweka Bajeti kubwa sana katika Sekta hizo na amewaahidi Watanzania wategemee makubwa katika Sekta hizo. Lakini vile vile ameahidi kufanya mageuzi kwenye sekta ya elimu ili iwe na tija zaidi na iwe yenye kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiajili zaidi kuliko kutegemea kuajiliwa.
Mhe. Samia amewataka Wananchi wa Tabora kuendelea kulinda misitu kwani uhai hutegemea misitu hiyo na amesisitiza kwamba hatotoa eneo jingine tena la hifadhi kwa Wananchi bali Wanachi wapunguze mifugo na wafuge michache yenye tija sana kuliko mingi ambayo haina tija.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Rais amewataka Viongozi wote hususani wa Mikoa na Wilaya kuongeza jitihada zao katika usimamizi wa fedha kwenye miradi ya maendeleo, lakini sambamba na hilo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini waongeze jitihada kwenye kukusanya mapato kwani kiwango bado hakiridhishi sana na zaidi ya yote watoe taarifa kwa UMMA juu ya fedha zinazokuja kwa kutaja ni kiasi gani, kwa mradi upi ili waweze kufuatilia utekelezaji wake.
Na Katika matumizi ya fedha za maendeleo, Rais Samia ameagiza taratibu zote za kisheria za matumizi ya fedha zifuatwe na asiwepo mtu wa kukiuka hata kidogo, na kwa ngazi ya Halmashauri amesisitiza kwamba Baraza la Madiwani ndio linapanga matumizi yote ya fedha za maendeleo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.