Na Alex Siriyako,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefungua rasmi barabara ya Nyahua mpaka Chaya Mkoani Tabora. Barabara hii yenye kiwango cha lami imegharimu zaidi ya Bilioni 123 ikiwan ni kipande kimojawapo katika barabara kuu inayotoka Mkoani Tabora kwenda mpaka Itigi Mkoani Singida. Barabara hii imeweza kujengwa kwa hisani ya Mfuko wa Maendeleo wa Nchi ya Kuwait.
Hafla ya uzinduzi wa barabara hii imeshuhudiwa na Viongozi mbalimbali, Wageni waalikwa pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Tabora hususani Kata ya Tura Wilayani Uyui ambapo zoezi la uzinduzi limefanyika. Miongoni mwa wageni na Viongozi waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Buriani, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait Ndg. Marwan A. Al-Ghanem, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Tabora, Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Tabora, Wabunge wa Majimbo ya Mkoa wa Tabora, Viongozi wa Dini, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Tabora.
Mhe. Rais amewashukuru sana Wananchi wa Mkoa wa Tabora kwa mapokezi yao mazuri, hii ikiwa ni ziara yake ya kwanza Mkoani Tabora akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Amewashukuru Kuwait kwa mchango wao mkubwa kwa maendeleo ya Tanzania na amewapongeza wadau wote walioshiriki katika mradi huu pamoja na kuahidi kumaliza mapema sana miradi yote iliyoanzishwa Awamu ya Tano.
Mhe. Rais amepokea changamoto mbalimbali za Wilaya ya Uyui na Mkoa wa Tabora kwa Ujumla ikiwa ni pamoja na uhaba wa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari, Changamoto ya malipo ya Tumbaku kwa Wakulima ambayo hayajalipwa, Uhaba wa Matundu ya vyoo Mashuleni, Changamoto ya fidia kwa Wakazi ambao maeneo yao yametwaliwa katika ujenzi wa mradi wa kupeleka umeme Mkoani Kigoma kutokea Tabora na kwa ujumla wake ameagiza Mawaziri husika kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo changamoto hizo na pale watakapokwama wamuone.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Buriani katika kutoa Salamu za Wanatabora pamoja na Utambulisho, amemshukuru Mhe. Rais kwa kutupatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa muda mfupi sana akiwa madarakani hususani fedha za UVIKO-19, ambapo zimefanikisha ujenzi wa madarasa mengi sana, umaliziaji wa Vyuo Vya VETA pamoja na Ujenzi wa Miundombinu ya Maji. Mwisho amemhakikishia Mhe. Rais kwamba Tabora tunatambua jitihada zake na tunapambana sana kumuunga mkono katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Nchi yetu.
Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait Ndg. Marwan A. Al-Ghanem nae alipata wasaa wa kusalimia Wanatabora na amesema uhusiano kati ya Tanzania na Kuwait kwenye miradi ya maendeleo umeanza zamani sana toka mwaka 1975 na mpaka sasa Serikali ya Kuwait imefadhili miradi yenye thamani zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 285. Ameahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Kuwait na amewashukuru wadau wote katika ujenzi wa barabara ya Nyahua-Chaya.
Aidha katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Rais ametoa maagizo kwa Mawaziri hususani Wziri wa Maji pamoja na TAMISEMI kuhakikisha kwamba tenda zilizobaki katika matumizi ya fedha za UVIKO-19 zimalizike haraka iwezekanavyo na kufika June mwaka huu wawe wamemaliza zoezi hilo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.