Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa, amesema Serikali ya Tanzania kupitia kwa Mhe. Rais Samia Sluhu Hassan inatambua umuhimu wa michezo nchini kama moja ya fursa za kiuchumi kwa wanamichezo.
Mhe. Kassim Majaliwa amesema hayo leo Agust 04, 2022 Mjini Tabora, wakati akizungumza katika ufunguzi rasmi wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2022 yanayofanyika kitaifa Mkoani Tabora.
Katika hotuba yake Mhe. Waziri Mkuu ameeleza kuwa Rais Samia alikubali Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2022 kufanyiaka kutokana na kutambua umuhimu wa michezo na wanamichezo nchini kwa kuzingatia kuwa michezo ni ajira.
“Rais anatambua na ameahidi kuendelea kuongeza ubora wa miundo mbinu ya michezo mashuleni ili kuzidi kutengeneza mazingira bora ya wanafunzi kushiriki michezo mbalimbali”
“Wanamichezo wameanza kuhamasika kushiriki michezo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi, na hii yote inachangiwa na nia njema ya serikali katika kukuza na kutangaza michezo kuanzia katika ngazi ya chini” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema kuwa michezo na sanaa ni ni moja ya stadi muhimu kwa wanafunzi, ndio maana serikali imekuwa ikiwekeza fedha nyingi katika mashindano ya UMITASHUMTA, UMISETA na mashindano ya vyuo vya ualimu ambayo hufanyika kila mwaka.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea na mpango wake wa kuboresha michezo mashuleni kwa kuwaajiri waalimu wa michezo ambapo tayari jumla ya waalimu 83 wameshaajiriwa lengo ikiwa na kuzidi kuinua sekta ya michezo nchini.
Awali akimkaribisha Waziriki Mkuu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Elimu) Ernest Silinde alieleza kuwa wanamichezo zaidi ya elfu tatu kutoka mikoa yote nchini wanashiriki katika mashindano ya UMITASHUMTA 2022 Tabora wakiwa wanawakilisha michezo mbalimbali.
Silinde amesema kuwa mipango ya serikali iliyoanza ya kuboresha miundo mbinu ya viwanja mbalimbali vya michezo nchini vikiwepo vile vya mashuleni, inaenda kuibua wanamichezo wengi mahiri watakaliwakilisha vema Taifa kimataifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batlida Buriani, ameishukuru Serikali kwa kuuchagua mkoa wa Tabora kuwa mwenyeji wa UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2022, jambo ambalo amesema limezidi limezidi kuuheshimisha mkoa huo.
Amemualeza Waziri Mkuu kuwa mashindano hayo yameuchangamsha mkoa wa Tabora kibiashara, na kusaidia uchumi wa watu mbalimbali kuongezeka kutoka na huduma zinazotolewa kwa wageni waliokuja kushiriki michezo.
Katika maombi yake kwa waziri Mkuu, Balozi Dkt. Batlida Buriani aliomba michezo hiyo iendelee kuandaliwa Tabora kwa mwaka unaofuata, ombi ambalo waziri mkuu wakati wa kuhitimisha hotuba yake, alisema limekubaliwa hivyo UMITASHUMTA na UMISSETA 2023 itafanyika tena Tabora.
Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2022 yaliyofunguliwa rasmi leo Agust 4,2022 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, yanasimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Utamaduni, Sanaana Michezo.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.