Na Alex Siriyako:
Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamisi Mohamed Mwinjuma ameupongeza Mkoa wa Tabora kwa maandalizi mazuri ya michuano ya UMITASHUMITA na UMISSETA Kitaifa kwa awamu ya pili mfululizo.
Mhe. Mwinjuma amesema kuwa Tabora inastahili pongezi kwani imefanya vyema sana katika maandalizi ya michezo hii latika sekta zote.
Mhe. Naibu Waziri ametoa pongezi hizi leo akifungua rasmi michuano ya UMISSETA Kitaifa inayoendelea katika Viwanja vya Tabora Boys na Tabora Girls, Mkoani hapa leo Juni 15, 2023.
Aidha Mhe. Mwinjuma amemshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake kubwa sana za kukuza sekta ya michezo Nchini, jitihada ambazo anazionesha kwa vitendo mathalani zawadi ambazo amezitoa kwa vilabu vya Simba na Yanga katika michuano ya Kimataifa.
Mhe. Naibu Waziri ameendelea kufafanua kuwa msingi wa mashindano haya ni kuibua vipaji na kuviendeleza katika viwango vikubwa vya Kitaifa na Kimataifa.
Mhe. Naibu Waziri ameeleza pia kuwa Serikali ya awamu ya sita katika kuendeleza michezo Nchini imeanza ukarabati wa miundombinu ya mochezo katika shule 56 kutoka mikoa yote Nchini ambapo takribani shule mbili kila Mkoa zitapata fursa hii.
Katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Mwinjuma ameeleza kuwa Sanaa ni chombo pekee cha kutunza utamaduni wetu, Sanaa inaleta kipato kwa mtu binafsi, jamii na Taifa kwa ujumla, lakini pia Sanaa hutumika kutangaza kampeni mbalimnali za Kitaifa na Kimataifa.
Pamoja na kufungua mashindano haya, Mhe.Mwinjuma amepata fursa ya kukagua ubora wa viwanja vinavyotumika katika michuano hii.
Mwisho
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.