Na Alex Siriyako:
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mheshimiwa Ramadhani Kapela amesisitiza wafanyabiashara katika Manispaa ya Tabora kufuata bei elekezi ya sukari, kwani bidhaa hii imepata changamoto nyingi sana za kupanda bei kiholela ikiwa ni pamoja na kuadimika kabisa katika siku za hivi karbuni.
Mhe.Kapela amesema haya leo Machi 6,2024 katika kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili mwaka wa fedha 2023/2024, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora.
Amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Kilimo na Mifugo, imechukua hatua za kutosha na madhubuti kukabiliana na upungufu wa sukari Nchini, na kwa sasa uhaba huo umepungua kwa kiasi kikubwa, sukari ipo hivyo Wafanyabiashara wafuate bei elekezi ya sukari ambapo kwa Manispaa ya Tabora kwa sasa jumla kilo ni Tsh.2800 na rejareja ni Tsh.3000.
Halkadhalika, katika Baraza la Madiwani lililofanyika leo, Waheshimiwa Madiwani wamewasilisha taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kata zote 29 za Manispaa ya Tabora ,ambapo miradi ya maendeleo inayotekelzwa katika kata hizo imebainishwa, lakini pia na changamoto ambazo bado Wananchi wanakabiliana nazo zimeelezwa.
Katika kuhitimisha Baraza hilo, Mhe.Kapela amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia fedha nyingi za maendeleo Manispaa ya Tabora hususani sekta ya Afya, Elimu pamoja na Miundombinu na kuahidi kuwa fedha hizo zitasimamiwa ipasavyo kuhakikisha kuwa kazi zilizokusudiwa kufanyika zinakamilika.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.