Na Alex Siriyako:
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Kapela ameitaka Menejimenti ya Manispaa ya Tabora kwa ujumla wake kuwathamini sana wafanyabiashara ndogondogo mathalani mama lishe na machinga na wasibugudhiwe katika shughuli zao kwa sababu ya aina yeyote.
Mhe. Kapela ametoa maelekezo haya leo machi 7, 2024, katika kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili mwaka wa fedha 2023/2024, kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora.
Amefafanua kuwa hivi karibuni amepata malalamiko ofsini kwake kutoka kwa wajasiriamali wadogowadogo hasa mama lishe wakilalamikia kuondolewa katika maeneo wanayofanyia biashara huku wakidai kuwa wameambiwa maeneo walipo sio mahala sahihi kwa biashara zao, wakielezwa kuwa wapo maeneo ya hifadhi za barabara ama kwenye mifereji ya maji.
Mhe. Kapela amefafanua kuwa anatambua kuwa kuna mama lishe na machinga ambao kiuhalisia hawako maeneo sahihi, akaeleza kuwa lazima busara itangulie kwanza katika kufanya maamuzi yeyote, hivyo ameelekeza machinga ama mama lishe wasisumbuliwe, waachwe wafanye kazi zao, wapate riziki zao na kama kuna eneo watalazimika kuondolewa basi utaratibu mzuri wa kuwaondoa utatumika kwa ushirikiano wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Mhifadhi Seif Salum, amemshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Manispaa ya Tabora kiasi cha bilioni moja na milioni mia moja (1,100,000,000/=) kwa ajili ya kununua vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya na amesisitiza kwamba Manispaa ya Tabora itazisimamia vyema fedha hizo katika kuhakikisha kwamba vifaa tiba vinanunuliwa na vikiwa na ubora unaotakiwa.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.