Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Maiga Nyanja akiambatana na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Shabani Kapela pamoja na wadau wa ujenzi wa vyumba vya madarasa 69 wamekutana na Wakuu wa Shule za Sekondari hususani Shule ambazo zimepata fedha za madarasa kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuweka mikakati ya kujenga vyumba vya madarasa 69 ya kidato cha kwanza vyenye thamani ya Tzs. 1,380,000,000/= (Bilioni Moja, na Milioni Mia tatu themanini tuu) ikiwa ni mgawo kwa Manispaa ya Tabora ambapo uwiano wa darasa moja kwa milioni ishirini.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa, ambapo kimejumuisha wadau wote wa Ujenzi wakiwamo Mafundi ujenzi, Wazabuni, Watendaji Kata, Mafundi wa thamani, Wakuu wa Shule ,pamoja na Menejimenti ya Manispaa ya Tabora. Aidha Wadau wamekumbushwa kuwa kufikia January shule zinapofunguliwa watoto wa kidato cha kwanza wanatakiwa kutumia madarasa haya.
Aidha katika kikao kazi hiki, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela kwa nafasi yake amesisitiza kuwa kila mradi uwe na fundi mmoja, na fundi mmoja asiwe na miradi miwili kwani kufanya hivo kutapunguza kasi ya utekelezaji wa mradi na kuchelewesha kazi.
Vilevile Mstahiki Meya amewataka Watendaji Kata hususani kwenye vikao vyao vya WDC wawahimize Wananchi kushiriki na kuweka nguvu zao kwenye miradi hii kazi ya kuchimba msingi na kuweka kifusi na mawe kwenye msingi iwe sehemu ya nguvu kazi zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja katika maelekezo yake amewataka Wakuu wa Shule waunde Kamati za ujenzi na ununuzi kwa kufuata miongozo inavyotaka na kusisitiza wanakamati hao pindi wanapopatikana wapewe mafunzo ya kuwawezesha ili wafanye shughuli zao kwa weledi mkubwa.
Dkt. Nyanja amewataka Wakuu wa Shule kuleta taarifa ya utekelezaji kwa kila hatua ya ujenzi kabla ya malipo kufanyika na kuongeza kuwa baada ya hapo atatuma timu yake ya ukaguzi kwenda kukagua ubora wa mradi kwa hatua hiyo lakini vilevile kupata thamani halisi ya malipo yanayoombwa.
Vilevile Mkurugenzi amewaomba Mawakala wa vifaa vya ujenzi wawe waadilifu na wazalendo, wasitumie mwanya huu kupandisha bei za vifaa vya ujenzi hususani saruji, nondo, bati nk ambavyo ndio vifaa muhimu sana kwa ujenzi wa madarasa. Aidha Mkurugenzi ametumia fursa hiyo kuwaomba wazabuni wa madini ya ujenzi kutopandisha bei ya madini hayo kwa kivuli cha ujio wa fedha hizi za madarasa.
Aidha Dkt.Nyanja amewataka mafundi ujenzi kuongeza ubunifu na jitihada katika kazi zao na amesema hategemei kukuta ukuta ama sakafu imepasuka kwa sababu yeyote ile ya kiufundi, huku akiongeza kuwa mafundi milango watumie Mbao kavu za miti migumu lakini vilevile milango na madawati vipigwe Vanishi na Msasa kabla ya kukabidhiwa.
Katika kuhitimisha kikao kazi hiki, wajumbe wote waliohudhuria wamekubaliana kwa pamoja kuwa ujenzi uanze rasmi mnamo tarehe 16 mwezi October na ukamilike kufikia tarehe 15, mwezi Disemba mwaka huu 2022
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.