Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala leo tarehe 5.9.2019 amezindua rasmi kampeni yake ya kujenga madarasa 128 yatayogharimu kiasi cha Tshs. 2.3 bilioni yenye jumla ya tofali 177,000 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Katika kampeni hiyo pia itajumlisha shule tatu za Sekondari ambazo zitajengewa mabweni ya wasichana kwa lengo la kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu na kuwaepushia wasichana vishawishi vya njiani waendapo au watokapo shuleni.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika kwenye viwanja vya kituo cha Afya cha Maili tano kilichopo Ipuli Manispaa ya Tabora, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala alisema kampeni hiyo inatokana na harambee aliyoianza miezi mitatu iliyopita na kupata kiasi cha shilingi million 380 zikiwa ni fedha taslimu na ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali wa Elimu.
Katika uzinduzi huo Komanya alisema kuwa kuna shule tatu zitajengewa mabweni ya wasichana kwa lengo la kuwaondolea adha wasichana kukwepa vishawishi njiani waendapo au kutoka shuleni. Ambapo kwa kuanzia alimkabidhi Afisa Elimu Kata ya Itetemia Jashia Maarufu jumla ya tofali 1481 kwa ajili ya muendelezo wa ujenzi wa mabweni.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Kata ya Itetemia Jashia Maarufu, alisema wanamshukuru sana Mkuu wa Wilaya kwa kuja na wazo ambalo litakuwa mwarubaini wa shida ya majengo ya madarasa na mabweni kwa Shule za Mnaispaa na kwa maana nyingine kampeni yake Mkuu wa Wilaya ya kuipaisha Manispaa Kielimu itafanikiwa kuliko hata walivyotarajia. Hivyo akatumia fulsa hiyo kuwaomba wananchi na wadau wote kumuunga mkono Mkuu wa Wilaya ili kuweza kufikia lengo la kuifanya kila nyumba ya mwana Manispaa kuwa na Muhitimu wa Chuo Kikuu.
Aidha kwa upande wao mafundi wanaofyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo,walisema kwao imekuwa ni fursa nzuri kwani sasa wana uhakika wa kuingiza kipato kutokana na kazi ya ufyatuaji matofali.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.