Mkuu wa wilaya ya Tabora, Mheshimiwa Dkt.Yahya Ismail Nawanda akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Meya wa Manispaa Tabora, amefanya kikao chake cha kwanza na watumishi wote wa Halimashauri ya Manispaa ya Tabora wakiwemo Makatibu Tarafa.
Katika kikao hicho alipata fursa ya kuwafahamu watumishi waliohudhuria kikao hicho na vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora aliweza kutoa taaarifa fupi kwa Mkuu wa Wilaya yenye takwimu za idadi ya kata, vijiji, idadi ya wakazi pamoja na vijiji vya wilaya ya Tabora.
Aidha Mustahiki Meya wa Manispaa Tabora alipata fursa ya kuzungumza machache, alimkaribisha sana Mkuu wa Wilaya, na kumhakikishia ushirikiano wa kutosha na kwa muda wote ambao atakuwa anamuhitaji. Vilevile Mustahiki Meya alimuomba Mkuu wa Wilaya kwa nafasi yake atafute mbinu ya kumaliza na kutokomeza hoja ya hati chafu ya Mkaguzi wa hesabu za serikali kwa Manispaa ya Tabora.
Mkuu wa Wilaya ambae amewahi kuwa mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida na Mhadhiri katika chuo kikuu cha Sokoine(SUA), kwa nafasi yake aliwashukuru wenyeji wake kwa kumkaribisha, alimshukuru pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kumuamini na kuahidi kwamba hatomuangusha, atatekeleza majukumu yake kwaniaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kutekeleza Ilani ya chama cha Mapinduzi.
Katika hotuba yake fupi, Dkt. Yahaya amewasihi watumishi wa Halimashauru ya Manispaa ya Tabora kuwa wamoja, watiifu, wenye hofu ya Mungu, wenye upendo baina yao na kwa wananchi, wafanye kazi kwa weledi na waogope fedha za umma. Amesisitiza pia kwamba kila mmoja katika jamii ana kipawa chake alichopewa na Mungu ataheshimu mawazo ya kila mtu. Lakini pia amehimiza miradi yote iliyoanzishwa itekelezwe na ikamilike.
Dkt.Yahaya alibainisha vipaumbeele vyake kwa ufupi kwa sasa ambavyo ni pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato, amesema hawezi kukubaliana na hati chafu kwa Halimashauri anayoiongoza yeye na katika hilo ameahidi kufumua na kuunda upya Idara ya Fedha. Kipaumbele chake kingine ni kutatua kero za wananchi kwani ndio kazi kubwa ya viongozi na watumishi wengine wa umma. Amewataka vilevile kila mtumishi kuwa na mpango kazi wake kwa kila mwezi na wafuge kuku kwa niaba ya kuongeza vipato.
Aidha Mheshimiwa mkuu wa Wilaya aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa halimashauri ya Manispaa ya Tabora na kwenda kuutembelea na kukagua mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Tabora. Alifika na kupewa maelezo mbalimbali ikiwemo thamani ya mradi ambayo utagharimu zaidi ya Bilioni moja na milioni mia nne za kitanzania, ambapo kwa sasa mradi ushatumia zaidi ya milioni mia saba. Vilevile alielezwa kwamba malengo ya Hospitali ni kufikia Mwezi wa nane mwaka huu Idara ya huduma ya wagonjwa wa nje (OPD) ianze kufanya kazi.
Mkuu wa Wilaya alimaliza kwa kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Ndg. Bosco Nduguru kufuatilia kwa ukaribu na kuhimiza ujenzi uende haraka kwani wananchi wanahitaji huduma na magojwa hayana subira.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.