Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amefungua maonyesho ya nane nane leo tarehe 05-08-2019 kwa kanda ya Magharibi kwa kuwataka wakulima,wafugaji na wavuvi wa kanda ya Magharibi kuhakikisha bidhaa zao wanazoleta kwenye maonyesho hayo ya nane nane zina uhalisia kwa maana ya kwamba ni zile zinazozalishwa na wao wenyewe binafsi au kutoka kwenye vikundi vyao halisi na siyo kununua kutoka masokoni na kuletya hapo kwenye maonesho.
Akiongea kwenye uzinduzi huo mbele ya umati mkubwa uliofurika kwenye viwanja hivyo vya nane nane vilivyopewa jina la FATUMA MWASA vilivyopo Ipuli Manispaa ya Tabora Mkuu wa Mkoa alisema, kwenye maonesho hayo hakuna nafasi ya kudanganya kwamba unaenda kuleta bidhaa zilizozalishwa na watu wengine na kuja nazo ili kuzionyesha katika banda lako,hayo siyo makusudio ya ya maonyesho haya,alisema Mwanri.
Alibainisha kwamba , kama wakulima watafuata maelekezo yote yanayotolewa na wataalam wetu na kuzingatia mbinu za kisasa za kilimo, uvuvi na ufugaji utakuwa ni wenye tija sana na kwamba bidhaa zao zitapendwa sana na kila mtu atakayekuja kutembelea kwenye mabanda yao ataweza kununua na kujifunza pia.
Aidha alitoa agizo kwa maafisa kilimo, mifugo na uvuvi wa kanda ambayo inajumlisha Mikoa ya Kigoma na Tabora kufanya ukaguzi kwenye mabanda yote ili kujiridhisha kama bidhaa zilizopo eneo la maonyesho zinazalishwa na wahusika wenyewe na kuzifanyia tathimini ya kiwango cha ubora unaotakiwa.
Nae mwakilishi wa Wizara ya Kilimo kutoka Makao Makuu ndg Sospeter Wambura alisisitiza kuwa maonyesho ya nane nane mwaka huu yamepewa kauli mbiu inayotaka Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kuwa ni yenye kuleta tija na maendeleo kwa ukuaji wa UCHUMI WA NCHI.
Wambura akawataka wakulima, wafugaji na wavuvi kuwa wabunifu na wazingatie maelekezo ya wataalamu ili waweze kunufaika na utalaamu huo unaotolewa kwao, na waache ujanja ujanja kwenye shughuri zao za uzalishaji wa bidhaa ili waweze kukuza uchumi wao na kwa Taifa pia.
Awali kwenye ufunguzi huo wa maonyesho ya nane nane, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Komanya Kitwala amabe ndiyo mwenyeji wao alisema kuwa, ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wameyachukua na watayafanyia kazi. Aidha aliwataka wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na washiriki wote kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu ili waweze kunufaika na shughuri zao ili ziwaongezee uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Maonyesho ya nane nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Fatuma Mwasa vilivyopo Ipuli Manispaa ya Tabora ambayo mkilele chake kitakuwa tarehe 8/8/2019, yatafungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia mstaafu Emmanuel Maganga.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.