Maonesho ya nane nane kwa mwaka 2019 yamefungwa rasmi leo tarehe 8/8/2019 kwenye viwanja vya Fatuma Mwasa hapa Ipuli Manispaa ya Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Mstaafu Emanuel Maganga huku akiwataka Ofisa Kilimo wote kutokaa ofisini kwao, badala yake waende kutoa elimu kwa wakulima wa vijijini ili waweze kubadilika na kuwa wakulima wa kisasa.
Akizungumza jana wakati wa kufunga maonesho ya nane nane Kanda ya Magharibi yaliyofanyika hapa hapa Manispaa ya Tabora, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alisema kuwa kutopata elimu ya kutosha kwa wakulima wetu kumechangia sana kutofanya vizuri hasa kwenye uzalishaji na hivyo kutokuwa na mazao yaliyo bora zaidi.
Kadiri muda unavyozidi kwenda ndivyo ubora wa mazao ya wakulima unazidi kuwa wa kiwango cha chini sana kwenye ubora na hata wingi wa mazao yenyewe pia hasa kwa wakulima ambao waliowengi wanapatikana kwenye vijiji vyetu.
Alisema kuwa, wakati wote serikali imekuwa ikisisitiza sana kuwa Kilimo ndio uti wa mgongo. Maana yake ni kwamba wataalamu sasa waisaidie serikali kwenda kutoa elimu kwa wakulima huko waliko vijijini, waondokane na tabia za kukaa ofisini wkahamasishe na kuelimisha matumizi sahihi ya kanuni za kilimo bora na matumizi sahihi ya pembejeo zikiwemo mbegu ili kufanya wakulima wapate mavuno yaliyo bora na mengi zaidi kwa wakati mmoja.
RC Maganga alishangaa kuendelea kuwaona Ofisa Ugani walio wengi wakiendelea kukaa ofisini licha ya serikali kuagiza waende kwenye mashamba ya wakulima kuwasaidia, agizo ambalo bado halijatekelezeka kwa ukamilifu zaidi. Utakuta wamelundikana ofisini tuu huku wakiwaacha wakulima peke yao huu ni uzembe, alisema Maganga.
Nawaagiza Ofisa kilimo wote waende wakakae na wakulima wao ili walete mabadiliko yenye ari mpya ya kilimo bora na chenye tija. Na yeyote atayekaidi agizo hili atachukuliwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aidha alisema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbali mbali za kuboresha kilimo ikiwemo kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati zaidi ili kuifanya sekta hiyo iweze kuzalisha malighafi zitakazotumika viwandani na hivyo kuweza kulipatia mapato zaidi Taifa na kuwainua wakulima wote kiuchumi na dhamira ya serikali iweze kutimia kwa wananchi wake.
Hatuwezi kukaa kimya wakati wakulima wetu hawapati msaada wowote kutoka kwa Ofisa ugani, ni lazima hatua zichukuliwe ili kufanya maonesho yajayo yawe na mabadiliko makubwa na wakulima walete bidhaa zenye ubora wa hali ya juu zaidi.
Maonesho ya nane nane kwa Kanda ya Magharibi mwaka huu yalifanyika kwenye viwanja vya Fatuma Mwasa vilivyopo Manispaa ya Tabora yakiwa na kauli mbiu ya KILIMO,MIFUGO NA UFAGAJI KWA UKUAJI WA UCHUMI WA NCHI.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.