Na. Alex SIRIYAKO:
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imetoa mikopo ya vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu yenye thamani ya Tsh.1,632,818,500/= katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Mikopo hii imetolewa leo Januari 4, 2025 katika viwanja vya Manispaa ya Tabora, ambapo Mgeni rasmi katika Hafla hii alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Ndugu Deusdedith Katwale ambaye amewakilishwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora Bi. Asha Churu. Hafla hii imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Madiwani wa Manispaa ya Tabora, Wakuu wa Divisheni na Vitengo pamoja na wanufaika wa mikopo.
Awali, akitoa taarifa ya uratibu wa mikopo hii, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Tabora Bi. Tumaini Mgaya ameeleza kuwa, Manispaa ya Tabora ilitenga kiasi cha Tsh.1,632,818,500/= kwa ajili ya mikopo hii ya asilimia kumi kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, fedha ambazo zimekopeshwa kwa jumla ya vikundi mia moja arobaini na nane (148), sawa na asilimia nne (4%) kwa vikundi vya vijana, asilimia nne (4%) kwa vikundi vya wanawake na asilimia mbili (2%) kwa vikundi vya watu wenye ulemavu.
Aidha, Bi. Tumaini ameongeza kuwa, jumla ya vikundi vilivyoomba mikopo hii vilikuwa 235, ambapo viliomba mikopo yenye thamani ya Tsh. 5,448,487,472/= na kulingana na fedha iliyotegwa kuwa haitoshelezi mahitaji ya vikundi vyote, vikundi vingine vyenye sifa na vile ambavyo havikuwa na sifa vimekosa mkopo huo kwa awamu hii.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora Bi. Asha Churu akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Deusdedith Katwale amewataka wanufaika wa mikopo hii kwenda kuitumia vyema mikopo hii ili iweze kuwainua kutoka hatua waliyonayo sasa na kwenda hatua nyingine ya kiuchumi.
Aidha, Bi. Churu amemshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha mikopo hii kutolewa, kwani bila idhini yake vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wa vikundi hivi 148 wasingeweza kupata fedha hizi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela kwa upande wake amewasisitiza wanufaika wa mikopo hii kuwa mikopo hiyo sio zawadi ama hisani kwao, amefafanua kuwa mikopo hiyo ni mikopo kama ilivyo mikopo ya benki, tofauti yake ni kwamba mikopo hii haina riba na dhamana yake ni nafuu ila urejeshwaji wake ni wa lazima ili vikundi vingine vipate fursa ya kunufaika na mkopo huo.
Ndugu Ramadhani Nassoro ni mlemavu wa ngozi, ambaye amenufaika na mkopo wa milioni 80, ambazo pamoja na mambo mengine, amenunua lori la kubebea madini ujenzi aina ya FUSO FIGHTER, kwa upande wake pia amemshukuru sana Rais Samia kwa kuwapatia mikopo hii na ameahidi kuwa kwa upande wake binafsi anakwenda kupiga kazi na atarejesha mkopo huo kwa wakati.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.