Na Alex Siriyako:
Hafla ya kukabidhi fedha hizi imeshuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe.Louis P. Bura ambae amekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya mia nne thelathini na saba milioni na laki tatu (437,300,000/=) kwa vikundi arobaini na nne (44) ,ambapo vikundi 18 ni wanawake ambao wamepata 159,000,000/=, vikundi 16 ni Vijana na wamepata 260,000,000/=, na vikundi 10 vya watu wenye ulemavu ambao nao wamepata 18,300,000/=. Hafla ya kukabidhi mikopo hii imefanyika katika ukumbi wa White Sand uliopo Kata ya Chemchem karibu na Soko Kuu leo Machi 14, 2023.
Aidha kabla ya kuwakabidhi mfano wa hundi hiyo yenye thamani ya pesa tajwa hapo juu, Mhe. Bura aliwausia wanufaika hawa wa mikopo kuwa waadilifu sana na Mikopo hii. Mhe. Bura amewaeleza kuwa mikopo hii sio zawadi kwao na kuongeza kuwa ni sharti irejeshwe kwa utaratibu uliowekwa ili na Watanzania wengine wapate fursa ya kukopa mikopo hii isiyo na riba kabisa kwani uhitaji ni mkubwa sana.
Vilevile Mhe. Bura amewapa nasaha kina mama kuwa wawe na busara kwenye ndoa zao kwani wengine wamekuwa jeuri kwa waume zao hasa baada ya kujiimarisha kiuchumi, amewasihi sana watumie akili na busara nyingi sana kulinda ndoa zao na kuongeza kuwa mikopo ipo kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa familia zetu.
Aidha Mhe. Amrani Kasongo ambae ni Diwani wa Kata ya Chemchem , Manispaa ya Tabora ametoa nasaha zake baada ya kupata wasaa wa kuwasalimia wanufaika. Mhe. Kasongo amewasihi wanufaika wakaishi maisha ya mkopo na sio maisha ya kama fedha ni za kwao. Mhe. Kasongo ameongeza kuwa kinachowatesa wakopaji wengi hata kwene taasisi zingine za kifedha ni kuanza matumizi ambayo sio sahihi ya fedha za mkopo ,hivyo baada ya hapo huanza kuhangaika kwenye marejesho.
Katika kuhitimisha hotuba yake fupi kwa wanufaika hawa, Mhe. Bura amemshukuru sana Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo kwa Manispaa ya Tabora na Wilaya ya Tabora kwa ujumla wake.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.