JUMLA ya shilingi milioni 80.5 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya uwezeshaji kwa vikundi 14, ikihusisha vikundi 13 vya wanawake na kikundi 1 cha vijana.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Sheria inayozitaka Halmashauri kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani kwa ajili mikopo ya uwezeshaji wa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akikabidhi hundi za mikopo leo kwa vikundi hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Erick Kitwala Komanya alisema fedha walizokopeshwa zinapaswa kutumika kama chachu ya kuwaletea maendeleo.
Alisema fedha walizokopeshwa wanapaswa kuzitumia katika malengo waliyoombea na siyo kupeleka katika matumizi mengine kama vile starehe na anasa ambazo zitawafanya washindwe kurejesha.
Mhe. Komanya aliongeza kuwa wanatakiwa kurejesha fedha hizo kwa wakati ili vikundi vingine vya vijana , wanawake na walemavu waweze kukopeshwa kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na jamii inayowazunguka.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Leopold Chundu Ulaya alisema kuwa mikopo waliyopewa haina riba kwa hiyo wanapaswa kurejesha fedha kulinga na kiwango walichopata.
Naye Naibu Meya Yahaya Mhamali alisema lengo la mikopo inayotolewa ni kuwakomboa vijana, wanawake na walemavu kutoka umaskini na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Nchi.
Alisema kuwa kikundi kitakachorejesha mkopo kwa wakati kitapewa mkopo mwingine zaidi ya ule walioupata awali.
Hadi kufikia sasa Manispaa ya Tabora imeshatoa milioni 226 kwenye mwaka huu wa fedha 2018/2019 ikiwa ni mikopo ya vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.