Na Paul Kasembo-TMC
Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imefanya Semina kwa Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Watendaji kwa lengo la kuwapa elimu juu ya ujio wa zoezi la Anwani za Makazi ili kuwawezesha kuwa na uelewa mkubwa zaidi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Akifungua Semina hiyo Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja aliwaeleza wajumbe juu ya dhamira ya Manispaa kuwaita hapo, kwamba Serikali inakusudia kuendesha zoezi la Anwani za Makazi kwa Nchi nzima.
Ambapo kwa Manispaa ya Tabora pia inatarajia kuanza utekelezaji hivi karibuni, na ndiyo sababu ya kuitwa kwa wajumbe hao ili kuweza kupeana uelewa wa jambo linalofuata.
“Tumeita hapa ili tuweze kuoeana uelewa wa jambo ambalo tunatarajia kwenda kulitekeleza sote kwa pamoja kwenye maeneo yetu ya kiutawala, na kwamba kwenye hili zoezi viongozi wangu niwaombe tukalitekeleze kwa kutanguliza uzalendo mkubwa zaidi, umakini, usahihi na kwa wakati zaidi ili tuweze kufika malengo ya Serikali ya kumtambua mtu alipo na kuwezesha huduma za kijamii kumfikia kirahisi”, alisisitiza Dkt. Nyanja.
Kando na utangulizi huo, pia Mkurugenzi wa Manispaa aliwataarifu Wenyeviti hao kuwa atakuwa na utaratibu wa kukutana nao angalau maea mbili kwa mwaka ili kuweza kujadili juu ya namna bora ya kuboresha huduma kwa wananchi huku akiwataka kutumia mikutano hiyo kujadili changamoto zinazo wakabili na namna ya kuzitatua kwa pamoja.
Kwa upande wake mgeni wa mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda, aliwashukuru sana Wote waliohudhuria huku akiwashukuru zaidi wenyeviti wote kwa namna ambavyo wamekuwa wamekuwa wakimpatia ushirikiano wakati wote.
Dtk. Nawanda aliwaeleza wajumbe kuwa, Serikali ya Wilaya imejipanga vyema kwenda kulitekeleza zoezi la Anwani za Makazi kwa wakati, kwa weledi, kwa ufanisi mkubwa sana na kwa umakini ili Wilaya ya Tabora iwe ya kwanza kwa kutekeleza kwa kuzingatia yote hayo na hatimae iwe ya kwanza ki-Mkoa na ki-Taifa pia.
“Viongozi wangu hamjawahi kuniangusha hata mara moja, nina imani kuwa hata kwenye hili tunakwenda kulitekeleza vizuri zaidi na tuatakuwa wa kwanza kwa kila kitu, sina shaka nanyi hata kidogo”, alisema Dkt. Nawanda.
Kukamilika kwa zoezi hili kunatajwa kuwa na tija sana, ambapo kutawezesha sasa kuwa na uwezo wa kupeleka maendeleo, miundombinu ya kijamii na kuweza kutambua wapi anapatikana na hivyo inakuwa rahisi zaidi kumfikia kwa ajili uokozi, kupeleka huduma, na hatimae kumfikia kirahisi na kwa wakati.
MWISHO.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.