Halmashauri ya Manispaa ya Tabora imeelezea mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita ambayo yanaonekana waziwazi katika Manispaa ya Tabora ambayo yamekuwa na tija kubwa sana kulinganisha na kipindi kama hiki kwa awamu zilizopita.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja alipokutana na waandishi wa vyombo vya habari mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Manispaa ya Tabora.
Dkt. Nyanja aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, amewaita ili waweze kusaidia kuihabarisha umma na wa-Tanzania kwa ujumla waweze kujuwa kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na inayoendelea kutekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Manispaa ya Tabora.
“Kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Rais wetu, Mama yetu, Kiongozi wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan tumepokea fedha zote za ruzuku kama zilizvyotengwa kutoka Serikali Kuu kwenye eneo la LCDG, TOZO (Dev Foreign) na FEDHA ZA NJE (Dev Foreign), hii inakuwa kwa mara ya kwanza kwa Halmasahuri ya Manispaa ya Tabora kupokea fedha zote za ruzuku ya miradi ya maendeleo kutoka fedha za ndani zilizotengwa kwenye bajeti ukilinganisha na awamu zilizopita.” alisisitiza Dkt. Nyanja.
Pia Halmashauri ya Manispaa ya Tabora inaishukuru sana Serikali ya Awamu Sita chini ya uongozi wa mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kipekee za kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Moja kati ya mifano halisi ni huu wa fedha za UVIKO-19 ambapo kwa Manispaa ya Tabora tulipatiwa gawiwo la shilingi 1,573,485,741,91 fedha ambazo zilitumika kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa 60 kwa Sekondari, na vyumba vya madarasa 14 kwa Shule Shikizi ikiwa ni pamoja na uendeshaji wa Chanjo ya UVIKO-19” Dkt. Nyanja.
Kwa upande wa Utawala Bora, kwa kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan Manispaa ya Tabora imefanya zoezi la upandishwaji na ubadilishwaji vyeo kwa watumishi 653 kutoka Idara mbalimbali na wale waliobadilishiwa vyeo (recategorization) ni 99 na wameishabadilika vyeo vyao kwenye mfumo wa Lawson. Watumishi wote hao waliopandishwa vyeo walibadilishiwa mishahara yao ndani ya mwezi mmoja tuu na sasa wanaendelea kufurahia Serikali yao, kwakuwa hakunatena malimbikizo makubwa ya mishahara.
Pia Halmashauri ya Manispaa ya Tabora iliajiri watumishi 79 ikiwa ni ajira mpya kabisa kwa Idara ya Elimu Msingi, Elimu Sekondari, Afya, Ujenzi, na Idara ya Utawala na Utumishi.
Aidha Manispaa imeendelea kutekeleza agizo la uwezeshaji makundi maalum kama Serikali ilivyoelekeza, na kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita Manispaa ya Tabora imeweza kutoa mikopo kwa vikundi 129 vya wanawake, vijana na wenye ulemavu na kwamba jumla ya shilingi 662,500,000/= imetolewa.
Ambapo wanawake vikundi 99 vilikopeshwa shilingi 516,000,000/=, vijana vikundi 15 sawa na shilingi 118,000,000/=, na watu wenye ulemavu ni vikundi 15 vimekopeshwa shilingi 28,500,000/= na jumla kuu inakuwa shilingi 662,500,000/=.
Utoaji wa taarifa za mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ni sehemu ya utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, sambamba na utoaji wa shukurani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha na kuweka mazingira rafiki kwa wajasiliamali wadogo wadogo.
MWISHO
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.