NA PAUL KASEMBO
HALMASHAURI ya Manispaa ya Tabora imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 884 ambayo ni sawa na asilimia 18 ya makadirio ya kukusanya bilioni 4.6 ya mwaka wa fedha 2021/2022.
Takwimu hizo zimetolewa leo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Alisema makusanyo hayo ni miezi miwili ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha unaoendelea.
Dkt. Nyanja alisema lengo la Manispaa ni kuhakikisha kabla ya kumalizika kwa robo ya kwanza Halmashauri iwe imekusanya asilimia 25 ya makisio na kufikia bilioni 1.1.
Alisema mafanikio hayo yameanza kuonekana baada ya kubadilisha watumishi waliokuwa wakihusika na ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuongeza nguvu ya ukusanyaji kwa kubuni vyanzo vipya vingine.
Dkt. Nyanja aliongeza kuwa mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha huu Manispaa inatarajia kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ya kiasi cha milioni 100.
Aidha Dkt. Nyanja amevitaka vikundi vinavyokopeshwa fedha kuhakikisha vinazitumika katika kuimarisha mitaji yao ili wawaachie fursa watu wengine kunufaika na mikopo.
“Ifike wakati vikundi hivi vinavyokopeshwa viwe vinahitimu ili kutoa fulsa kwa vikundi vipya na vyenyewe kupatiwa mikopo hiyo na mwisho wa siku vikundi vyote viwe vimenufaika kama maelekezo ya fedha hizo zinavyoelekeza badala ya kuwa vinajirudia rudia tuu vikundi hivyo hivyo,” alisisitiza Dkt. Nyanja.
Katika hatua nyingine Dkt. Nyanja alielezea namna ambavyo Manispaa imejipanga kutekeleza Miradi ya maendelo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Zahanati, vyumba vya madarasa, utengenezaji wa madawati na ukarabati wa baadhi ya majengo ya shule yaliyochakaa.
Ambapo alisema kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo kutatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri jambo ambalo litapelekea utoaji wa huduma kwa wananchi na kuboresha miundombinu ya mji na hivyo kuufanya mji kuwa na muonekano bora na mzuri zaidi kuliko awali.
“Tumejipanga kuongeza juhudi za ukusanyaji wa mapato jambo ambalo litapelekea kuendeleza ujenzi wa Zahanati zetu, ujenzi wa vyumba vya madarasa, uongezaji wa madawati kwa wanafunzi, ukarabati wa majengo ya shule yaliyochaa na uboreshaji wa utoaji huduma kwa wananchi wetu jambo ambalo litaongeza ustawi wa wananchi wetu pia,” alisema Dkt. Nyanja.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.