Mkuu wa Wilaya ya Tabora ,Dkt.Yahaya Nawanda amewataka Wataalamu wanaopata mafunzo ya kukusanya na kuweka taarifa za Anwani na Makazi kwenye Mfumo, wawe na heshima kwa Wakazi ikiwa sambamba na kuwasikiliza Wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Serikali, kwani woa ndio wenyeji wao na wanawafahamu vizuri wakazi wao na maeneo yao kwa ujumla.
Aidha Dkt.Nawanda amemshukuru sana Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, pamoja na fedha zingine za maendeleo ambazo ameshaipatia Wilaya ya Tabora, pia ameipatia Wilaya yetu fedha kiasi cha Tsh. 170,808,378.75 kwa ajili ya Operesheni ya Anwani za Makazi na Postikodi.
Dkt.Nawanda aliwasihi Vijana wakawe waadilifu na wafanye kazi kwa weledi mkubwa sana kwani maendeleo ya Tabora ni ya kwao na ndio maana Mh.Raisi wa Jamhuri ya Muungano aliagiza fursa hizi za ajira ziende kwa wenyeji,alikusudia wenyeji wanufaike na Mradi na pia wawe walinzi wakubwa wa miundombinu ya Mradi huu.
Ujumbe huu wa Mkuu wa Wilaya kwa Wanasemina ulitanguliwa na taarifa kutoka kwa Mratibu wa Operesheni ya Anwani na Makazi kwa Manispaa ya Tabora,Bi.Suzana P. Mizengo, ambae alitoa taarifa ya utekelezaji wa Opereshini hii mpaka sasa.
Bi.Suzana ameeleza kuwa mpaka sasa kazi kubwa ya kuelimisha UMMA imefanyika kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo Semina, Vyombo vya Habari pamoja na Vikao mbalimbali vya Halmashauri. Vilevile Mratibu ameeleza kwamba mpaka sasa Manispaa imefanya usaili kwa makundi matatu ya watu wanaohusika na utekelezaji wa zoezi hili(Waandikaji wa namba za nyumba,Wachoraji wa Vibao vya Majina ya Barabara pamoja na wakusanya taarifa za Mfumo wa Anwani za Makazi) ,Aidha Mratibu ameeleza kwamba mpaka sasa idadi ya nyumba/Majengo/viwanja 87,843 zimeainishwa na kupewa namba katika kata 29 za Manispaa ya Tabora.
Takribani watu 500 wamepata mafunzo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi (NaPA) ,Wakiwemo Watendaji wa Kata,Watendaji wa Mitaa na Vijiji, Pamoja na Wakusanya taarifa walioshinda kwenye zoezi la usaili.
HABARI PICHA
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.