Na Alex Siriyako
Bi. Happiness Madeghe, Mkuu wa Dawati la Uelimishaji Umma wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Tabora akiongea na Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Tabora katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani robo ya nne mwaka wa fedha 2023/2024 katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora amekumbusha kuwa kama Taifa tunaenda kwenye chaguzi mbalimbali kuanzia wenyeviti wa mitaa, vijiji na Vitongoji mwaka huu, pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais mwakani, hivyo suala la rushwa limekuwa ni changamoto kubwa hasa ifikapo nyakati hizi za uchaguzi.
Bi. Madeghe amefafanua kuwa, rushwa iko katika mazingira tofauti tofauti sana, ikiwemo rushwa ya kutoa fedha taslimu, rushwa ya ngono, pamoja na rushwa ya kutoa zawadi ya aina yeyote ili tu mlengwa aweze kutimiza adhima yake, hivyo amesisitiza kuwa TAKUKURU iko kazini masaa ishirini na nne, na kwa kipindi hiki cha uchaguzi itaongeza nguvu zaidi, pia amewasihi sana Waheshimiwa waendelee kuwaelimisha Wananchi wao madhira yatokanayo na vitendo vya rushwa.
TAKUKURU, TUWASA, TANESCO pamoja na TARURA ni miongoni mwa taasisi za umma zinazotoa huduma katika Manispaa ya Tabora ambazo zimealikwa na kupata wasaa wa kutoa ufafanuzi, elimu pamoja na mpango mkakati wa kuendelea kumaliza changamoto za Wananchi hasa kwenye maji, umeme pamoja na barabara.
Kwa upande wao Waheshimiwa Madiwani,pamoja na mambo mengine, wamesisitiza hasa upande wa TARURA kuwa, taratibu za kuwapata wazabuni ziharakishwe, ili angalau vipande vilivyopata bajeti kwa mwaka huu wa fedha, viweze kuanza kujengwa kabla nvua hazijaanza kunyesha, lakini pia waendelee kufanya jitihada za kurekebisha barabara zilizosombwa na nvua nyingi msimu uliopita, kwani nazo barabara hizi kwa sasa hazipitiki kabisa.
Aidha, Waheshimiwa Madiwani wameendelea kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Manispaa ya Tabora fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo hasa katika sekta mtambuka za Kilimo, Elimu, Afya pamoja na Miundombinu ya barabara.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela kwa niaba ya Baraza ametoa pongezi za dhati kwa Menejimenti ya Manispaa ya Tabora chini ya Uongozi wa Mkurugenzi wa Manispaa hii Ndugu Elias M. Kayandabila kwa kukusanya mapato kwa asilimia mia moja kwa mwaka wa fedha 2023/2024, lakini pia kwa kupata hati safi ya ukaguzi wa CAG kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.