Na Alex Siriyako:
Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora leo Januari 13, 2025 katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora, wameridhia na kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026, ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora inatarajia kutumia kiasi cha fedha za Kitanzania Bilioni hamsini na moja milioni mia tano tisini elfu ishirini na saba, mia tatu kumi na moja na senti mbili (Tsh.51,590,027,311.20 ).
Waheshimiwa Madiwani wamefikia maamuzi haya baada ya kupokea rasimu hii na kupitia vyanzo vya mapato ya fedha hizi sambamba na mgawanyo wa matumizi ya fedha hizi hasa mgawanyo wa fedha za miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya Rasimu ya Bajeti, Afisa Mipango wa Manispaa ya Tabora Ndugu Nelson Mwankina amefafanua kuwa, katika kiasi hiki cha zaidi ya bilioni hamsini na moja, ruzuku kutoka Serikali Kuu ni shilingi 43,883,178,704.00, na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ni shilingi 7,706,848,607.00, na katika bajeti hii shilingi 13,865,612,464.32 ni fedha za miradi ya maendeleo na kiasi kingine cha fedha kikibaki kuwa mishahara ya Watumishi na matumizi mengineyo ya ofisi.
Akifungua kikao hiki cha Baraza Maalumu la Madiwani la Bajeti, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela ameeleza kuwa roho ya Halmashauri ni mapato, na amesema kuwa hatamfumbia macho mtu yeyote atakayekuwa kikwazo kwenye makusanyo ya mapato ya Halmashauri.
Katika kutilia Mkazo wa ujumbe wake, Mhe. Kapela ameagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuchukua hatua kwa mtumishi/watumishi Idara ya Ujenzi ambao waliingizia hasara Halmashauri kwa kufanya makisio ya chini ya vibali vya ujenzi na kuisababishia Halmashauri hasara kubwa, na akaongeza kuwa, hakuna mfanyabiashara yeyote akatakwepa kulipa tozo na ushuru halali wa Halmshauri kwa jeuri ya fedha zake ama viongozi wakubwa anaofahamiana nao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Shani Mdamu, ambae ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Tabora, ameeleza kuwa, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora amepokea ushauri wote wa wajumbe na wanaenda kuufanyia kazi tena kwa wakati.
Mwisho.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.