Na Alex Siriyako:
Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama wameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa kutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta za Afya, Elimu, Miundombinu ya Barabara pamoja na Utawala Bora.
Madiwani wa Kahama wametoa pongezi hizi leo Disemba 23, 2024 katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora ambapo wamefanya ziara ya kujifunza katika Manispaa hii kwa siku mbili. Aidha pongezi hizi zimetolewa baada ya kupokea taarifa ya miradi ya kimkakati ambayo imetekelezwa, inayoendelea kutekelzwa na inayotarajiwa kutekelezwa na Manispaa ya Tabora.
Kadhalika ,Waheshimiwa Madiwani wa Kahama wamepata fursa ya kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo kama jingo jipya la utawala la Makao Makuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mtandao wa barabara za rami zilizojengwa chini ya mradi wa ULGSP chini ya ufadhili wa benki ya Dunia, lakini pia wakajionea namna ambayo miti iliyopandwa kuzunguka mji mzima wa Tabora inavyoupendezesha mji wa Tabora ukiachilia mbali faida zake zingine za kimazingira.
Mhe. Sindano Machumu, Naibu Meya wa Manispaa ya Kahama, kwa niaba ya Madiwani wa Kahama, ameishukuru sana Manispaa ya Tabora kwa mapokezi mazuri, ushirikiano mzuri na zaidi ya yote ameipongeza Manispaa ya Tabora kwa utunzaji mzuri sana wa miradi ya barabara pamoja na uhifadhi wa mazingira, “mji wa Tabora unapendeza sana hasa unapoowanisha barabara nzuri zenye miti inayomeremeta” Mhe. Mchumu amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Ndugu Robert Kwela, ameishukuru pia Manispaa ya Tabora kwa mapokezi mazuri, amefafanua kuwa wamejifunza mengi sana katika Manispaa hii, hasa namna ya kukabiliana na changamoto katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, namna ya kutunza mazingira, hasa upandaji wa miti, na zaidi yote ameeleza kuwa wanaenda kuyafanyia kazi yote waliyojifunza.
Kwa niaba ya Manispaa ya Tabora, Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Adam Kalonga ambaye aliambatana vilevile na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Shani Mudamu katika salamu zake amewapongeza na kuwashukuru sana Madiwani wa Kahama kwa kuja kujifunza Tabora, amefafanuwa kuwa mji wa Tabora ni mji wa asali na maziwa na wenyeji wa hapa ni wakalimu sana, hivyo wawe na amani kabisa.
Mwisho
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.