Na. Alex Siriyako:
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ndugu Mohamed Katete imeridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwa ni sambamba na ubora wa miradi hii katika Wilaya ya Tabora.
Kamati hii ya siasa imefanya ziara leo Januari 9, 2025 ya kutembelea na kukagua ubora wa miradi ya kimkakati katika sekta mtambuka Wilayani hapa, ambapo miradi kama Ujenzi wa Reli ya mwendokasi (SGR) kipande cha Makutupola, Singida hadi Tabora, Hospitali ya Manispaa ya Tabora, Ujenzi wa Uzio , Jengo la abiria na Maegesho ya magari katika Uwanja wa ndege Tabora, Shule ya Sekondari Malolo pamoja na Ujenzi wa Bwawa la Iyombo kijiji cha Tumbi.
Ndugu Katete kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tabora amemshukuru sana Mwenyekiti wa chama hicho Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi sana kwenye miradi ya maendeleo hasa sekta za Elimu, Afya ,Kilimo, pamoja na miundombinu ya barabara na Reli, ambapo wananchi wamesogezewa huduma pamoja na fursa za ajira kuongezeka.
Ndugu Katete amewaomba Wakazi wa Manispaa ya Tabora kuacha kwenda kupanga foleni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ( Kitete) kwani Dkt.Samia ameshatujengea Hospitali ya Manispaa ya Tabora ambayo inatoa huduma nyingi sana karibia na huduma zinazotolewa na Kitete,kwani utofauti wake ni mdogo sana, na amemshukuru sana Rais kwa kutenga fedha nyingi kujenga Hospitali hii pamoja na kununua vifaa tiba.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Tabora Ndugu Daniel Muhina, ameeleza kufurahishwa na ujenzi wa shule ya Sekondari Malolo sambamba na shule zingine za Sekondari Wilayani hapa kama Ifucha na Ntalikwa, aidha amesisitiza kwa niaba ya chama cha Mapinduzi kuwa fedha zilizoletwa kutekeleza miradi hii zitoshe kwa ubora uliokusudiwa, na miradi ikamilike huku wazabuni wote wakiwa wamelipwa.
Aidha wajumbe wa kamati hii wameridhishwa na kasi na ubora wa ujenzi wa uzio, jengo la abiria pamoja na maegesho ya magari katika uwanja wa ndege wa Tabora, ambapo ujenzi wa mradi huu uko mbioni kukamilika.
Kwa niaba ya Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Deusdedith Katwale, ameeleza kupokea ushauri na maelekezo ya Chama cha Mapinduzi, na ameahidi kupitia taasisi zilizopo chini yake kuwa watahakikisha ushauri huo na maelekezo ya chama yanatekelezwa kwa wakati.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.