BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora limelaani vitendo vya Polisi vya kuvamia Ofisi za Halmashauri wakiwa na silaha kwa lengo la kuwakamata watumishi wa umma ili kuwaweka ndani kwa maagizo ya baadhi ya viongozi.
Tamko hilo limetolewa leo na Mstahiki Meya wa Halamshauri ya Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhani Kapela (Diwani wa Kata ya Isevya) kwa niaba ya Waheshimiwa Madiwani wenzake wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri lilipokuwa likijadili utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa robo ya tatu mwaka wa fedha 2020/2021.
“Kumekuwepo na ukamataji wa watumishi wa umma hapa katika Ofisi za Halmashauri tena bila kufuata utaratibu, jambo hili limeleta shida hata kuwafanya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa uwoga, kukosa ari (moral) ya kufanya kazi, kufanya kazi chini ya viwango wakihofia kukamatwa. Sisi kama wasimamizi hatukabaliani na jambo hili” alisema Mstahiki Meya.
Alisema kufuatia vitendo hivyo kuendelea wao kama wasimamizi wa Halmashauri wamemwagiza Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Bosco Nduguru kumuandikia barua Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) wa Tabora ya kumtaka kufuata taratibu wakitaka kumkamata Mtumishi wa umma ambaye ameonekana kuwa na tatizo.
Mhe. Kapela alisema taratibu nzuri ni pamoja na kumtarifu Mwajiri wa Mtumishi, pia hata Mkurugenzi mwenyewe awe na taarifa ya kuwa mtumishi wake anakamatwa na kisha yeye anaweza kuruhusu askari wamchukue au anaweza kumuamuru mtumishi aende kuripoti Polisi kwa ajili ya taratibu zinazofuata za Polisi.
Alisema vitendo vya Polisi kuja katika Ofisi za Halmashauri wakiwa na magari na silaha vinasababisha taharuki kwa watumishi wengeni kwa kuwa ukamataji huo unaonekana kama vile wanakwenda kukamata jambazi ama jangili.
Kapela aliongeza kuwa vitendo hivyo vimesababisha kushuka kwa morali ya watumishi kwa kuwa kila wanapoona gari la Polisi wanasubiri kuona kuwa ni zamu ya nani anayekamatwa, imekuwa kama sinema.
Alisema kimsingi wao kama Waheshimiwa Madiwani hawapingi kama Mtumishi akiwa na makosa kukamatwa lakini ni vema utaratibu ukafuatwa ikiwemo wa kumuita Polisi, kumtaarifu mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa na sio kumfuata na silaha.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.