Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa Bw. Bosco Ndunguru na Menejimenti yote kwa kukusanya mapato ya ndani zaidi ya sh bilioni 3 tofauti na miaka mingine iliyopita.
Wakiongea katika kikao cha baraza kilichoanza tarehe 29-31/ 07/2019, walisema kuwa katika mwaka wa fedha 2018/2019 Manispaa ilikuwa na lengo la kukusanya kiasi chaTsh bilioni 4.2 lakini imeweza kukusanya Tsh bilioni 3.4 hadi sasa sawa na asilimia 81 ya lengo lake.
Katibu na msemaji wa Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi ambae pia ni Diwani wa (CCM) kata ya Ndevelwa Mhe, Seleman Juma Maganga alisema kuwa mapato hayo ni ya kihistoria kwani tangu Halmashauri hiyo ianzishwe haijawahi kuvuna kiasi hicho cha fedha katika makusanyo yake ya ndani.
Alisema kuwa mapato ya mwaka huu yameonesha dhahiri kuwa kumbe Manispaa inaweza kukusanya zaidi ya makadirio yake kama Ofisi ya Mkurugenzi itashirikiana ipasavyo na Wataalamu wake kama walivyofanya sasa, alisema Maganga.
Maganga alitoa mfano wa mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo Halmashauri hiyo ilikadiriwa kukusanya Tsh bil 3.6 lakini ikakusanya Tsh bilioni 2.5 sawa na asilimia 70 tu. Na kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ilikadiriwa kukusanya Tsh bilioni 3.8 lakini ikakusanya Tsh bilioni 2.2 sawa na asilimia 60 tu, lakini mwaka huu wamefanya vizuri zaidi.
Alifafanua kuwa mapato ndio uti wa mgongo wa Halmashauri yoyote na serikali yoyote duniani inategemea mapato ili kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Hivyo hatua ya kupandisha zaidi makadirio hadi sh bil 4.2 na kufanikiwa kukusanya asilimia 81 ya kiasi hicho kumeiwezesha Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wake.
Kwa uapnde wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora ambae pia ni diwani wa (CCM) kata ya Ipuli Mhe, Leopold Ulaya alisema kuwa, kwa mwezi Juni pekee Halmashauri imeweza kukusanya zaidi ya Tsh milioni 500 ambayo ni sawa na asilimia 156 ya lengo la makusanyo ya mwezi. Hivyo akatumia fulsa hiyo kuwasisitiza Menejimenti kuongeza kasi zaidi ili waweze kufanya vizuri zaidi na zaidi na kufikia lengo lililowekwa.
Aidha katika taarifa hiyo iliyosomwa na kwa niaba ya Madiwani wa CCM ilisema kuwa mafanikio hayo yamechochewa na kasi ya utendaji na maelekezo ya Mhe Rais John Pombe Magufuli, ambaye aliagiza kila Halmashauri kuongeza kasi zaidi ya ukusanyaji mapato.
Kwa namna ya kipekee, Madiwani walimpongeza sana Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala kwa weredi, ufanisi na ubunifu wake katika utendaji kazi wake na hivyo wakamuagiza Mkurugenzi wa Manispaa amuandikie barua ya pongezi.
Akiongea na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Manispaa,Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa Bw Ndunguru alikiri kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa halmashauri kukusanya mapato mengi namna hiyo. Aidha alisema kilichowasaidia sana kuwa ni ushirikiano wa wataalamu, madiwani, takwimu sahihi za vyanzo vya mapato ya walipa kodi wote na kutumia kikosi kazi maalumu/special task force kwenye kazi ya makusanyo.
Mkurugenzi litaja sababu nyingine kuwa ni utoaji elimu kwa walipa kodi wote, kazi amabayo ilifanywa na Halmashauri kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA) Tabora Manispaa na kudhibiti mapato na matumizi ya Halmashauri ikiwemo ushirikiano mzuri wa usimamizi,ushauri na fuatiliaji kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw Aggrey Mwanri na Mkuu wa wilaya ya Tabora Manispaa Bw Komanya Kitwala.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.