Madiwani wa Manispaa ya Musoma wakiwa katika picha ya pamoja na Wenyeviti wa Kamati mbalimbali za Kudumu za Manispaa ya Tabora wakati wa ziara yao mkoani Tabora hivi karibu ambapo walikuja kujifunza uboreshaji wa vyanzo vya mapato, mazingira na upandaji wa miti pamoja na mambo kadhaa mengine.
Aidha Madiwani hao Manispaa ya Musoma wameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa juhudi zao katika ukusanyaji wa mapato upandaji na utunzaji mazingira, usafi wa mji na mitaa yote kwa ujumla.
Wametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa ziara yao ya mafunzo katika Manispaa ya Tabora ili kuona utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi.
Waliongeza kuwa usimamizi na ujenzi wa barabara za Manispaa ya Tabora kwa kiwango cha lami zinaweka mazingira mazuri kwa watu kutoka nje ya Mkoa kuwa rahisi kuwekeza katika sekta mbalimbali kwa sababu ya urahisi wa usafiri.
Nae Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora ambae alimuwakilisha Mstahiki meya ambae hakuwepo wakati wa ziara hiyo,aliwashukuru na kuwapongeza sana Madiwani wote na wataalamu wao wote walioongoza nao kwenye ziara hiyo kwa uamuzi wao wa kuja kujifunza kwenye Manispaa ya Tabora. Na pia akatumia fulsa hiyo kuwakaribisha tena wakati mwingine.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Bw Bosco Ndunguru aliwashukuru sana wote waliofika kwa ajili ya kujifunza, akiwa na imani kubwa kwamba kwa yote waliyojifunza wataenda kuyaboresha na kisha kuyatekeleza ili yawe na tija zaidi kwa maslahi ya wananchi wa Musoma na kwa maslahi mapana ya Mkoa wao wa Mara na Taifa kwa ujumla.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.