Na Alex Siriyako:
Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Bukoba wamekoshwa na mandhari nzuri, iliyopendezeshwa na miti kando kando ya kila barabara, mtandao mkubwa wa barabara za rami, na hali ya usafi katika mji wa Tabora.
Madiwani hawa wa Bukoba wamekiri haya leo Aprili 10, 2025 ambapo wametembelea kwa nia ya kujifunza katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wakiongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Mhe. Godson Gypson, Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini Mhe. Steven Byabato pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Y. Sima.
Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Bukoba wamepata wasaa wa kujifunza namna Manispaa ya Tabora inauweka mji wake katika hali ya usafi, namna Manispaa ya Tabora inakusanya mapato yake ya ndani, na ni mbinu zipi Manispaa ya Tabora inatumia kusimamia miradi yake ya kimkakati hasa miradi ya TACTIC.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Mhe. Byabato amewataka Wataalamu wa Manispaa ya Bukoba kunakili vizuri kila walichojifunza katika Manispaa hii ya Tabora na kueleza kuwa hayo ni maazimio ya ziara hii, na atahakikisha kwamba kila walichojifunza kinafanyiwa kazi.
Kdhalika Meya wa Manispaa ya Bukoba, Mhe. Godson Gypson, amewashukuru Manispaa ya Tabora kwa kukubali kuwapokea na kuwapa uzoefu wa namna wanavyopambana kukusanya mapato yao ya ndani na jinsi wanavyosimamia miradi yao ya TACTIC, aidha amewaomba Madiwani wa Bukoba wawe tayari kuungana na Wataalamu kukusanya mapato saiti bila kudai posho kama madiwani wa Tabora wanavyofanya.
Baada ya majumuisho ya ziara hii, Naibu Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Idd A. Kalonga, kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Kapela, amewashukuru na kuwapongeza Madiwani hawa wa Bukoba kwa kuichagua Tabora kuwa sehemu ya kuja kujifunza, na amewaomba sasa kile walichojifunza waende wakakifanyie kazi na watapata matokeo chanya kama walivyokusudia.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.