Na Alex Siriyako:
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tabora Bi. Asha Churu akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe.Louis Peter Bura katika kikao cha wadau wa maendeleo wa Wilaya ya Tabora,ametoa maelekezo ya Serikali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora kuandaa na kuratibu Kongamano kubwa lenye malengo mahsusi ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Manispaa ya Tabora na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Bi.Churu ametoa maelekezo haya leo Novemba 26,2023 katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora baada ya majadiliano ya kina na wadau wa maendeleo na kubainika kuwa utalii na fursa zake za kiuchumi katika Wilaya ya Tabora na Mkoa wa Tabora bado hazijatangazwa vya kutosha hivyo kuna sababu za msingi za kujipanga upya na kuzitangaza fursa hizo.
Wadau wa maendeleo wa Wilaya ya Tabora wamekutana leo katika ukumbi wa Manispaa ya Tabora huku wakiwa na ajenda kubwa ya kutangaza utalii wa Tabora, ambapo leo katika kikao hiki wamekutana na Balozi na Mdau mkubwa sana wa Utalii Tanzania Bi.Nangasu Werema ambae ameungana na wadau hawa leo katika kupeana uzoefu na mikakati inayoweza kutumika kutangaza Utalii na fursa zake za kiuchumi zinazopatikana Mkoa wa Tabora.
Bi.Werema ameeleza kuwa, kwasasa ana kampeni ya kutangaza Utalii wa Tanzania kwa jina la TALII NA MAMA SAMIA, kampeni yenye kauli mbiu isemayo UTALII NI UCHUMI. Ameendelea kufafanua kuwa kwasasa anatangaza vivutio vya Utalii kwa Mikoa ya Kanda ya Magharibi ambapo ameanza na Mkoa wa Tabora.
Miongoni mwa wadau waliohudhuria kikao hiki ni pamoja Mhifadhi Sefu Salumu ambae ni Afisa Maliasiri wa Manispaa ya Tabora na ameeleza kwa kina vivutio vya utalii katika Wilaya ya Tabora vikiwamo Tabora ZOO, Tembe la Dkt.Living Stone, Mnara wa Mwalimu Nyerere, Tabora School, pamoja na Njia Kuu ya Watumwa wakitokea Ujiji Kigoma hadi Bagamoyo.
Aidha Wawakilishi kutoka TANAPA Kanda ya Magharibi, TAWA Kanda ya Magharibi pamoja na TFS Wilaya ya Tabora walikuwepo na kila mmoja wao amepata nafasi ya kueleza vivutio pamoja na fursa za kiuchumi walizonazo mbele ya wadau waliohudhuria kiako hicho.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.