NA ALEX SIRIYAKO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Bw. Musalika Makungu kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batilda Buriani, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Katibu Tawala pia aliambatana na Wataalamu mbalimbali kutoka Sekiretarieti ya Mkoa, miongoni mwa watalaamu hao ni pamoja na Jacob Mnyambwa (Mchumi), Jiame M.Mbati (Katibu Tawala Msaidizi), Shani Mangesho (Msimamizi wa Fedha, Serikali za Mitaa) pamoja na Rukia Manduta (Katibu Tawala Msaidizi). Hali kadhalika katika ziara hiyo, Katibu Tawala aliweza kuongozana na Watalaamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wakiongozwa na Mkurugenzi wa Manispaa Dkt. Peter M. Nyanja.
Katika ziara hiyo miongoni mwa miradi iliyopata fursa ya kutembelewa ni pamoja na; Ujenzi wa Madarasa mawili na Ofisi (UVIKO-19) pamoja na ukarabati wa Maabara ya PHYSICS shule ya Sekondari Cheyo, Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Ujenzi wa madarasa matano na Ofisi moja (UVIKO-19), Ujenzi wa madarasa matatu na Ofisi moja(Mapato ya Ndani) shule ya Sekondari Ipuli, Mradi wa Upimaji Viwanja 24 Kata ya Mapambano pamoja na Mradi wa kujenga Vibanda vya Machinga eneo la karibu na Standi kuu ya Mabasi kata ya Chemchem.
Katika ziara hiyo, Miradi yote imekaguliwa kwa kina na kwa ujumla Wataalamu wa Mkoa walilidhika na ubora wa miradi yote ikiwa ni sambamba na kasi ya utekelezaji ambapo kwa mfano Hospitali ya Wilaya muda sio mrefu itaanza kutumika, na madarasa yote yamekamilika kwa asilimia zaidi ya tisini na tano. Wataalamu vilevile walifurahishwa na namna upimaji wa viwanja ulivyozingatia matumizi tofauti tofauti hususani uwepo wa Viwanja vya Viwanda Vidogo vidogo, kwani Tabora inahitaji Viwanda sana kwa sasa. Hali kadhalika alihimiza ujenzi wa Vibanda vya Machinga uongeze kasi na mabanda hayo yapangwe kimkakati ili kuwe na mpangilio mzuri wa huduma katika soko hilo.
Aidha kulingana na changamoto ndogondogo zilizobainika, wataalamu wa Mkoa walitoa ushauri wao wa msingi sana ikiwa ni pamoja na kufuata Mwongozo wa PPRA katika kutekeleza Miradi hii inayojengwa kwa utaratibu wa Force Account, Bidhaa zote zinazonunuliwa na kupokelewa zionekane kwenye Kitabu cha REJA, Taarifa zote za miradi ziwepo kwenye mafaili zikiwemo taarifa za Mikataba ya Mafundi pamoja na taarifa za manunuzi.
Baada ya kumaliza kutembele miradi hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Bw. Musalika Makungu aliweza kuweka msisitizo kwenye maelekezo ya Wataalamu na ushauri wao,ikiwa ni pamoja na kufuata Mwongozo wa PPRA kwenye utekelezaji wa miradi yote inayojengwa kwa mfumo wa Force Account, lakini pia amesisitiza suala la Madawati yawepo kwenye madarasa yanayojengwa na zaidi kabisa akasisitiza kwamba uaminifu na uadilifu kwenye utekelezaji wa miradi ni wa razima. Mwisho kabisa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri aendelee kusimamia kwa weredi mkubwa miradi yote ndani ya Manispaa ya Tabora.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.