Na Alex Siriyako;
Kata ya Ng’ambo iliyopo Manispaa ya Tabora, katika Mkoa wa Tabora, ni miongoni mwa Kata mbili zilizoteuliwa kwa zoezi la Majaribio la kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura huku Kata nyingine ikiwa ni Kata ya Ikoma iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoani Mara.
Taarifa hizi zimebainishwa na Mhe. Balozi Omar Ramadhan Mapuri ambae ni Mjumbe wa TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI katika Mkutano wa Tume na Wadau wake ambao umefanyika leo Novemba 20, 2023 katika ukumbi wa Mwanakiyungi ,Mkoani Tabora, zoezi litakalo fanyika kuanzia Novemba 24 hadi 30,2023.
Mhe.Mapuri ameeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria za Uchaguzi, ni jukumu la Tume kuboresha Daftari la kudumu la Mpiga Kura kabla ya Uchaguzi mwingine kufanyika, na katika kuboresha mifumo na tekinolojia ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga kura kuna majaribio ya kutosha yanafanyika ili kubaini changamoto zote zinazoweza kujitokeza mathalani ubora wa vifaa vinavyotumika, mtandao hafifu wa simu, ukosefu wa umeme na kadhalika, ili changamoto hizi ziweze kufanyiwa kazi kabla ya zoezi kuanza rasmi.
Aidha Mhe.Mapuri amefafanua kuwa uboreshaji wa majaribio utahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au Zaidi, Raia atakae fikisha miaka 18 kabla au siku ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine, Waliopoteza kadi zao za kupiga kura ama kuharibika, Wanaorekebisha taarifa zao, pamoja na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria Tume ya Taifa ya Uchaguzi Ndugu Selemeni Mtibora akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI amefafanua kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa sana katika teknolojia itakayotumika kuandikisha wapiga kura ikiwa ni pamoja na BVR Kits mpya zenye kilo 15 badala ya zile za zamani za kilo 35, lakini pia zikitumia program endeshi ya ANDROID badala ya WINDOW.
Katika kuhitimisha Mkutano huu, wadau wameridhishwa na nia thabiti ya Serikali ya kuwashirikisha katika kila hatua hii na wameomba Serikali iendelee na utaratibu huo. Aidha wameeleza kuwa wako tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa zoezi la uboreshaji wa majaribio wa Daftari la Kudumu la Mpiga kura katika kata ya Ng’ambo linakwenda vizuri kama lilivyoratibiwa.
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.