Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Tabora ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambae pia ndio mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Wilaya ya Tabora Bw.Mohamed Katete akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dkt. Yahaya Nawanda, Mustahiki Meya Mh.Ramadhani Kapera, Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Dkt. Peter Nyanja, Katibu wa CCM, Wilaya ya Tabora Bi.Neema Lunga pamoja na wajumbe wengine wa kamati ya siasa wametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Akiongea na Wajumbe wa kamati,pamoja na Watendaji mbalimbali wa Serikali, Bwana Katete amemshukuru sana Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suruhu Hassan kwa upendo wake mkubwa kwa WanaTabora, kwamba ametupendelea sana kwa miradi yote anayotupa, vilevile amempongeza Mkuu wa Wilaya, Mh. Yahaya Nawanda pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Dkt. Peter Nyanja kwa usimamizi mzuri na wenye tija katika miradi yote hii ya maendeleo.
Miongoni mwa miradi iliyopata fursa ya kutembelewa na kukaguliwa ni pamoja na Ujenzi wa madarasa matano, ofisi moja kwa kiasi cha milioni mia moja, ujenzi huu ukitokana na fedha za Mpango Wa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, pia kamati ikakagua umaliziaji wa Boma la madarasa matatu na ofisi moja, ambapo Serikali imetoa milioni ishirini na tano, Hali kadhalika Kamati imekagua ukarabati wa Maabara unaotumia milioni thelathini ambazo ni fedha kutoka Serkali kuu. Miradi yote hiyo mitatu inatekelezwa kwenye Shule ya Sekondari Ipuli,Kata ya Ipuli.
Kamati imekagua Ujenzi wa Barabara kutoka Kakora kwenda Mwibiti,Barabara yenye urefu wa Kilometa 12 na inatarajia kugharimu kiasi cha Shilingi milioni miambili tisini na moja na laki tatu (291,300,000/=).Mradi huu umeanza Novemba 20 na unatarajia kukamilika May 2022.
Katita kata ya Misha, Kamata imeweza kukagua Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya kitakachogharimu kiasi cha milioni miambili na Hamsini (250,000,000/=) fedha kutoka Serikali Kuu, katika Mradi huu ambao ndio unaanza kutekelezwa, Kamati imetoa wito kwa Uongozi Halmashauri kuhakikisha kuwa Wananchi wanashirikishwa ipasavyo katika kila hatua. Vilevile kamati imesisitiza suala la usimamizi mzuri wa fedha za Serikali upewe kipaumbele.
Lakini pia Kamati imeweza kukagua Mradi wa Ujenzi wa Madarasa matano na Ofisi mbili katika Shule ya Sekondari Misha ambapo ujenzi uko hatua za umaliziaji.Kamati vilevile imemaliza kwa kukagua ujenzi wa madarasa sita, ofisi mbili katika Shule shikizi ya Usule, Kata ya Mbugani ambapo vilevile ujenzi uko hatua ya umaliziaji.
Bw. Katete, ambae pia ndio Mwenyekiti wa Kamati pamoja na kulidhika na ubora wa miradi amesisitiza ushirikishwaji wa Wananchi katika miradi yote hii ili waone umiliki wa Miradi yao, pia amesisitiza uadilifu na uaminifu katika usimamizi wa fedha hizi za miradi
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.Haki zote zimehifadhiwa.